0


UHURU
Wakati kamatakamata ya waganga wa kienyeji ikiendelea kupamba moto katika Mikoa mbalimbali hasa ya kanda ya ziwa, mmoja amenaswa na viungo vya binadamu kikiwemo kichwa ambacho bado kilikuwa na nywele zake.
Mganga huyo Nyamizi Magunga mkazi wa kijiji cha Igurubi Igunga,Tabora alitiwa mbaroni juzi ambapo mbali na viungo hivyo alikutwa na vifaa vingine ikiwemo nyara za serikali.
Mwenyekiti wa kijiji cha Igurubi George Henry alisema  Magunga alikamatwa nyumbani kwake wakati wa msako unaoendelea kwa ajili ya kuwabaini wanaofanya ramli chonganishi.
Msako huo unatokana na kukithiri kwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini ili kuwabaini na Serikali imekuwa ikisaka waganga hao wanaotumia ramli.
Henry alisema polisi hao walifanikiwa kumnasa mganga huyo kutokana na taarifa kutoka kwa raia wemo ambapo walipofanya msako walimkutana na vitu hivyo.
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete, ameitaka Wizara ya Utumishi ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi la  wa Umma kupitia Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu na Nyaraka, kufikiria uanzishwaji wa maktaba za marais ambazo zitakuwa zinahifadhi kumbukumbu zao.
Rais Kikwete aliyasema hayo wakati akifungua rasmi Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu na Nyaraka mjini hapa jana kilichojengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 7.9.
Alisema utunzaji wa kumbukumbu za marais waliomaliza vipindi vyao yakiwamo maandishi yao, ziara zao na mawasiliano na viongozi wengine duniani, utasaidia kuhifadhi historia ya marais hao.
Msipohifadhi historia ya marais wenu, mtakuwa mmepoteza kumbukumbu kubwa ya taifa lenu, alisema na kutoa mfano wa maktaba kama hizo nchini Marekani ambazo zinahifadhi kumbukumbu za magazeti yote duniani likiwamo gazeti la Ngurumo la Tanzania.
Alisema Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu ambacho kimejengwa kwa lengo la kuhifadhi kumbukumbu zake kwa dijitali, kina uwezo wa kuhifadhi mafaili zaidi ya 750,000, hivyo kitumiwe kuanzisha maktaba hizo.
Alisema Tanzania Bara imebahatika kupata marais katika vipindi vinne hivyo kama zingewekwa kumbukumbu kuanzia za rais wa awamu ya kwanza, itakuwa imehifadhi historia nzuri kwa vizazi vijavyo kwa kuwa watakuwa wanajuwa kila rais alikuwa na fikra gani katika uongozi wake.
Akizungumzia kituo hicho, Rais Kikwete alisema kitasaidia kuhifadhi kumbukumbu na kupunguza tatizo la ucheleweshaji wa malipo ya pensheni kwa sababu ya kukosa kumbukumbu nzuri na pia kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi na upotevu wa mali ya umma kwa kuwa kumbukumbu zote zitakuwa zinahifadhiwa kidijitali.
NIPASHE
Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya, ameendelea kuitolea ufafanuzi kauli maarufu ya‘kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe’ aliyoitoa wakati akiwasilisha bajeti bungeni miaka 25 iliyopita alipokuwa Waziri wa Fedha enzi za utawala wa serikali ya awamu ya pili, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi.
Msuya alitoa ufafanuzi huo katika mjadala kuhusu “Dira ya Maendeleo”  jijini Dar es Salam jana, ulioandaliwa na kituo huru cha kuhifadhi nyaraka zilizokusanywa na waandishi wa Bayografia ya Mwalimu Nyerere ili zitumiwe na watafiti, kijulikanacho kama Kavazi la Mwalimu Nyerere (NRC), kilichoanzishwa ndani ya Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).
Alikuwa akijibu swali la mmoja wa washiriki wa mjadala huo, Prof. Mwesiga Baregu, ambaye alimuuliza Msuya kwamba haoni kuwa kauli yake hiyo inaweza kuwa ndiyo chimbuko la ubinafsi nchini na kwamba inatofautiana na mtazamo wa Mwalimu Nyerere wa kuwataka Watanzania kubeba “msalaba wa taifa”, akihimiza ujamaa miongoni mwao.
Akijibu swali hilo, Msuya alisema kauli yake haikukusudia kupinga ujamaa, bali ilikuwa ikipinga hoja za kundi la wabunge waliokuwa wakilalamikia tozo ya kodi kwenye bidhaa, zikiwamo khanga.
Msuya alisema wabunge hao, ambao hawezi kuwataja, katika hoja zao walidai kuna watu wameoa wake watatu, hivyo tozo ya kodi katika khanga ingewafanya washindwe kumudu kuwanunulia wake zao vazi hilo.
Alisema hoja hiyo ndiyo iliyomfanya atamke kauli hiyo kwa sababu kuoa ni jambo la hiari ya mtu na kwamba, Mungu alikwishawaamuru wanamume kuoa mke mmoja, hivyo anayetaka kuwa na mke zaidi ya mmoja shauri yake atabeba jukumu hilo mwenyewe.
Awali, akielezea Kavazi la Mwalimu Nyerere, Mkurugenzi wake, Prof. Issa Shivji, alisema kuna mengi katika urithi ulioachwa na Mwalimu Nyerere, ambayo yamesahauliwa na kupuuzwa na Watanzania.
Hata hivyo, alisema kuna jambo moja lililojengeka katika hulka ya viongozi, hasa wa kizazi cha kwanza baada ya uhuru, ambalo bado lipo, ingawa limeanza kufifia.
NIPASHE
Kamati maalumu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), imekamilisha kazi ya ugawaji wa majimbo 211 ambayo ni sawa na asilimia 88 kati ya majimbo yote 239, imefahamika
Wakati hayo yakiendelea, kamati hiyo imeshindwa kuafikiana katika majimbo 28 ambayo yanasubiri uamuzi wa wenyeviti wa vyama vinavyounda Ukawa, ambao watamaliza kiporo hicho mwezi huu.
Hatua hiyo imekuja baada ya viongozi wa juu wa umoja huo, kutangaza mkakati wa kusimamisha mgombea mmoja wa urais na kuachiana majimbo ya uchaguzi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Ukawa ni umoja ulioanzishwa Februari mwaka jana wakati wa Bunge Maalumu la Katiba, ukiundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kamati hiyo maalumu ya Ukawa, kilisema jana kuwa kwa muda wa wiki moja sasa, kamati hiyo imekamilisha kazi hiyo kwa kiwango kikubwa jambo ambalo limeelezwa linaweza kutoa upinzani mkali kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu.
Tumekutana mara kadhaa na kukubaliana kuachiana majimbo. Tulijadili katika hatua za awali, na sasa kazi imekamilika kwa asilimia 88 na kubaki asilimia 12 ambayo itaamuliwa na wenyeviti.
“Majimbo 28 ambayo tumeshindwa kupata mwafaka tunaamini kamati ya kitaifa ya Ukawa inayoundwa na wenyeviti ndiyo itatoa dira ya nini kifanyike, ingawa sisi kama kamati maalumu tumekamilisha kazi yetu.
Kamati ilitafiti namna gani bora ya kuachiana madiwani, wabunge na rais ili tusimamishe mgombea mmoja katika kila eneo, lakini tulivutana kwani kila upande uliangalia masilahi yake, ingawa katika suala linaloitwa la ushirikiano ni lazima ukubali kupoteza sehemu na ninaamini Ukawa sasa itakuwa imara zaidi,kilisema chanzo chetu.
MWANANCHI
Serikali imewasilisha bungeni muswada wa Sheria ya Udhibiti wa Ajira za Wageni kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa ajira za wageni nchini, ikiwamo kuwabana wanaofanya kazi bila kuwa na elimu stahiki.
Hata hivyo, muswada huo ulipingwa na baadhi ya wabunge huku wengine wakiishauri Serikali kuorodhesha kazi zinazostahili kufanywa na raia hao wa kigeni ili kuepusha baadhi ya waajiri kuajiri watu kutoka nje kwa kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania.
Wabunge hao walionyesha kushangazwa na vitendo vya raia wa kigeni kuingia nchini na kujiita wawekezaji kwa kuuza maua na vikombe, kazi walizodai zinaweza kufanywa na Watanzania.
Muswada huo uliwasilishwa na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka ambaye alisema sheria hiyo itaweka sheria moja itakayoratibu na kurahisisha upatikanaji wa vibali vya ajira za wageni kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji na kuongeza uwajibikaji katika soko la ajira nchini.
Kabaka alisema kwa sasa kuna sheria nyingi zinazotoa ajira kwa wageni ambazo ni; Sheria ya Uhamiaji Namba Saba ya mwaka 1995, Sheria ya Wakimbizi Namba Tisa ya mwaka 1998 na Sheria ya Uwekezaji Tanzania (TIC) Namba 26 ya mwaka 1997.
Nyingine ni Sheria ya Mamlaka ya Maeneo Huru ya Uwekezaji (EPZA) Namba Tatu wa mwaka 2006, Sheria ya Usajili wa Biashara Namba 14 ya mwaka 2007, Sheria ya Elimu Namba 10 ya mwaka 1995 na Waraka wa Utumishi wa Umma Namba Moja wa mwaka 2000.
Waziri Kabaka alisema sheria hiyo itakuwa juu ya sheria zingine zinazohusu ajira za wageni na Serikali imeitunga kutokana na kuwapo kwa sheria zinazotoa mianya ya wageni kufanya kazi nchini bila kuwa na elimu stahiki.
Akichangia muswada huo ikiwa ni mara yake ya kwanza baada ya kutangazwa na chama chake kuvuliwa uanachama, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe aliitaka Serikali isiwe na haraka ya kuupitisha kuwa sheria kwa sababu haijajipanga kuwawezesha Watanzania watakaokosa ajira nje ya nchi kupata ajira nchini.
MWANANCHI
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amesema uchaguzi wa Rais ajaye utakuwa na ushindani mkubwa ndani na nje ya CCM, huku akibainisha kuwa haogopi mtu kati ya wote wanaotajwa kwenye kinyang’anyiro hicho, bali anawaheshimu.
Lakini mbunge huyo wa Singida Kaskazini amesema mgombea pekee atakayemwogopa ni yule atakayekuwa anataka kulipiza kisasi dhidi ya wagombea wengine.
Waziri huyo alitoa kauli hiyo jana wakati alipofanya ziara kwenye makao makuu ya Ofisi za Mwananchi Communications inayozalisha magazeti ya The Citizen, Mwananchi na Mwanaspoti zilizoko Tabata Relini kando ya Barabara ya Mandela.
Sipendi kulizungumzia sana jambo hilo,” alisema Waziri Nyalandu ambaye huzungumza kwa sauti ya chini na taratibu… “Kwenye chama chetu (CCM) muda wake bado. Lakini naweza kusema kuwa mwaka huu ni wa ushindani mkubwa ndani ya CCM na ‘opposition,” aliwaambia wahariri wa Mwananchi Communications.
Mwisho tutakuwa na kambi ya CCM. Kwaya ya CCM itapambana na kwaya nyingine ambayo ina sauti zote nne kama CCM,” alisema akimaanisha kuwa upinzani nao utakuwa umekamilika na kusisitiza muda ukifika atachukua fomu.
Kauli ya Nyalandu imekuja wakati nchi ikijiandaa kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu utakaoiweka madarakani Serikali ya Awamu ya Tano, hali ambayo inaipa shida CCM kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete ambaye pia atalazimika kuachia uenyekiti wa chama hicho.
Tayari wanachama wanne wa CCM wameshatangaza nia, akiwamo Nyalandu. Wengine ni Hamisi Kigwangala, ambaye ni Mbunge wa Nzega, January Makamba (Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia) na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
MWANANCHI
Siku tisa baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutangaza kumvua uanachama, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe jana alitinga bungeni na kufanya kikao cha siri na Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa zaidi ya saa moja.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watu walio karibu naye, mbunge huyo alipanga kuaga wabunge jana asubuhi baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, lakini baadaye alilieleza gazeti hili kuwa atazungumzia hatima ya ubunge wake leo.
Mbunge huyo ambaye pia jana alichangia mjadala wa Muswada wa Sheria ya Udhibiti wa Ajira za Wageni wa Mwaka 2014, alipowasili bungeni wabunge wengi walidhani angewaaga kutokana na taarifa zilizosambaa mjini hapa juzi kuwa angetumia siku ya jana kuaga lakini hakufanya hivyo.
Akizungumzia hali hiyo Zitto alisema: “Kuhusu mimi kuaga bungeni we subiri tu. Kama jambo hilo lipo litakuwepo tu. Ila kwa sasa, nimeitwa na Spika Makinda na ndiyo nakwenda kuzungumza naye.”
Aliongeza, “Si unaniona bwana, nimekuja bungeni na kama nisingekuwa mbunge nisingekuja. Nitazungumza tu, ila kwa sasa ngoja tuone mambo yatakavyokwenda.”
Hata hivyo, habari kutoka kwa watu walio karibu na Zitto zililieleza gazeti hili kuwa mbunge huyo atatoa kauli leo baada ya kushauriana na spika wa sasa, spika aliyepita, Waziri Mkuu wa sasa, waziri mkuu aliyepita, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Chadema, Said Arfi na washauri wake wa karibu kuhusu suala hilo.
Zitto alipoulizwa kuhusu hilo, alisema, “Aliyekueleza yuko sahihi, nitaongea kesho (leo) jioni kabla ya Bunge kuahirishwa ili kuweka wazi msimamo wangu kuhusu kinachoendelea kwenye ubunge wangu.”
Chadema ilitangaza kumvua Zitto uanachama siku tisa zilizopita, saa chache baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kutupa shauri lake alilofungua akitaka chombo hicho cha sheria kimlazimishe katibu mkuu wa chama hicho kumpa nyaraka za vikao vya Kamati Kuu vilivyomvua nyadhifa zote.
Awali, Mahakama hiyo ilitoa amri ya muda ya kuizuia Chadema kumjadili na amedumu kwenye nafasi ya ubunge chini ya zuio hilo kwa takriban mwaka mmoja.
Iwapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itapokea taarifa ya kuvuliwa kwake uanachama na kumjulisha Spika, Zitto atakuwa amepoteza kiti hicho.
MWANANCHI
Muuguzi wa Hospitali ya Mwananyamala, Pili Amiri aliyetekwa Machi 12, amepatikana usiku wa kuamkia jana baada ya watekaji hao kudaiwa kumtupa katika pori moja lililoko Dar es Salaam.
Hata hivyo, gazeti hili lilishindwa kufanya mahojiano na muuguzi huyo jana kwa kuwa alikuwa akihojiwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, kuanzia saa nne asubuhi hadi mwandishi alipoondoka kituoni hapo saa 11 jioni.
Kwa mujibu wa shangazi yake Pili, Fatuma Mbasa, muuguzi huyo alirudi nyumbani saa 10 alfajiri jana akiwa katika hali ya kulewa na makovu kadhaa shingoni.
Inaonekana walimpa dawa za kulevya kwa sababu alikuwa kama teja, hajiwezi na ana majeraha kadhaa na alikuwa akilalamika kuwa na maumivu shingoni,  Mbasa.
Alisema licha ya kuwa Pili alikuwa hawezi kuzungumza vizuri, lakini alisema watekaji hao walimpa mateso makali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema Pili pamoja na watu wengine saba wanahojiwa kuhusu tukio hilo.
“Kuna mambo mengi tumeyagundua kuhusu utekaji huu, lakini tutayaeleza baada ya kuwa tumeshawahoji. Ingawa amepatikana lakini hatuwezi kutoa ripoti nusu nusu,” Wambura
“Matukio ya utekaji yapo, sisi kazi yetu siyo kulifanyia kazi tukio hili moja, lakini tutahakikisha kupitia tukio la pili, tutajua kwa kina mchezo unavyofanyika na kuuzuia ili usijirudie tena.”
Mjomba yake Pili, Amiri Kangile alisema siyo kwamba familia hiyo ni ya watu wenye uwezo wa kifedha lakini waliamua kutoa kiasi hicho cha fedha kwa watekaji ili kumuokoa ndugu yao.
Alisema kwa mujibu wa maelezo ya awali ya Pili, watekaji hao walikuwa wakimwamuru akatoe fedha katika akaunti yake ya NMB akiwa chini ya ulinzi mkali.
HABARILEO
Wakati wadau wa usafiri nchini wakipendekeza kushuka kwa nauli za daladala na mabasi yaendayo mikoani, wamiliki wa mabasi wametishia kufuta utaratibu wa kutowatoza nauli askari na kuongeza kuwa, hata nauli pungufu za wanafunzi sasa zitakuwa historia.
 Wadau wamependekeza kupunguzwa kwa nauli za mabasi yaendayo mikoani kwa viwango vya kati ya asilimia 15 na 25 huku wakitaka nauli za daladala zipungue kutoka Sh 400 hadi Sh 300 kwa njia ya umbali wa kilometa 10.
Hayo yaliibuka jana wakati wa mkutano wa wadau kukusanya maoni kuhusu mapitio ya viwango vya nauli za mabasi ya mikoani na daladala kupungua kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta ulioandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
Katibu Mkuu wa Baraza la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra­ CCC), Oscar Kikoyo alisema sababu ya kutaka nauli kupungua licha ya kushuka kwa bei ya mafuta, pia wamiliki wa mabasi Julai mwaka 2014 walisamehewa ushuru wa forodha kwa asilimia 10 hadi 25 ya mabasi mapya yanayoingizwa nchini.
 Alisema mafuta yanachangia katika uzalishaji wa huduma kwa asilimia 20 hadi 30 na si jambo jipya katika kuomba kushusha nauli, kwani mwaka 2009 nauli ilishuka ambapo kwa nauli za kwenda mikoani wanataka ipungue kwa km moja kuwa Sh 28.05 badala ya sh 36.89.
Alitoa mfano wa nauli wanazotaka kwa mabasi ya kawaida kuwa Moshi na Arusha (Sh 17,000 badala ya Sh 22,700), Mwanza (Sh 32,369 badala ya Sh 42,000), Mbeya (Sh 23,365) badala ya sh 30,700), Bukoba (Sh 40,756 badala ya Sh 55,000) na Dodoma (Sh 12,678 badala ya Sh 16,700).
 Katika usafiri wa daladala wamesema wanataka iwe Sh 300 kwa kilometa kuwa Sh 31.39 kwa usafiri wa kilometa 10 badala ya Sh 400 na kilometa 15 iwe Sh 450 na maeneo mengine kupungua kwa Sh 100.
Kikoyo alisema pia wanaandaa ombi kupitia kanuni na sheria kwa wamiliki wanaotoza nauli kinyume inavyotakiwa walipishwe faini ya Sh milioni moja badala ya Sh 200,000 za sasa ili wayaone maumivu ya adhabu hiyo kubwa.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Mabasi ya Daladala (DARCBOA), Sabri Mabruk alisema wao wako tayari kupunguza nauli kwa asilimia mbili hata kesho kama walivyofanya
HABARILEO
Taasis ya Mashehe na Wanazuoni wa Kiislamu, imewataka maaskofu nchini wawe wavumilivu, kwani Serikali ni ya watanzania wote. Aidha, imewasisitiza watanzania kwa ujumla, kupata elimu ya Katiba Inayopendekezwa kwa kuisoma kwa makini na kuielewa ili wawe na uwezo na uhuru wa kuchagua kile wanachokiona kina manufaa kwao, bila kuwepo shinikizo la kiimani.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo, Shehe Khamis Mataka, wakati akitoa tamko la taasisi hiyo, kufuatia tamko la TCF kuhusu Katiba Inayopendekezwa, Mahakama ya Kadhi na Hali ya Usalama na Amani ya Nchi.
Tunawasihi watanzania wote kuendelea kudumisha undugu wao kama watanzania, bila kujali rangi, dini, kabila na itikadi za kisiasa na tumkemee yeyote yule anayetaka kutugawa kwa kutumia misingi ya kidini, kikabila, kisiasa na kiuchumi” alisema.
Pia, imeiomba Serikali iache kuzingatia tamko lililotolewa na Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF), badala yake iendelee na mchakato wa Katiba Inayopendekezwa na Mahakama ya Kadhi kwa kufuata misingi ya haki.
Shekhe Mataka aliongeza “Taasisi imezipitia kwa kina nukta zote nne za Tamko hilo pamoja na hitimisho lake na kubaini kwamba maaskofu wamejisahau kwamba wao ni viongozi wa kiimani na kiroho, ambao wanatakiwa wawe tayari kumpokea yeyote na kumpa neno la hekima lililojazwa faraja, bila hata ya kujali itikadi au chama chake cha siasa.
 Badala yake wameamua kutoa faraja kwa waumini wao kwa kuzingatia utashi wa kisiasa”. “Maaskofu wameamua kuanzisha utamaduni mpya wa kuendesha mambo ya kisiasa kwa misingi ya kiimani na hivyo kutoa tishio la kuwagawa watanzania kwa misingi hiyo.
Hivyo baada ya Taasisi yetu kujiridhisha na yaliyomo katika Tamko hilo la Maaskofu chini ya mwavuli wa TCF, tunashauri hatua za kuchukua,” alisema.
Alisema, “Kwa kuwa serikali ina vyombo makini vyenye wataalamu wenye uwezo wa kufahamu na kuelewa uvunjifu wa katiba na Umoja wa Kitaifa, tunaomba ipuuze tamko hilo ambalo limeisikitisha taasisi yetu na kuwadhalilisha waislamu.
“Suala la Mahakama ya Kadhi ni haki ya Waislamu na haliwahusu wala halihitaji ridhaa ya wasiokuwa Waislamu, kama ambavyo waislamu hawajapata kuombwa ridhaa yao katika yale ambayo Serikali imekuwa ikiwafanyia wakristo na makanisa yao,” alisema.
Shehe Mataka alisema, “Taasisi hii inapinga kwa nguvu zote madai ya Maaskofu kuwa, Waislamu kuwa na Mahakama ya Kadhi ni uvunjifu wa Katiba, kwani sheria za Kiislamu ni moja ya vyanzo vya sheria ya Tanzania.
Mahakama za Tanzania zimekuwa zikitumia sheria hizo kuhukumu kesi za waislamu kuhusu ndoa, talaka, mirathi toka mwaka 1963 na kufuatiwa na sheria ya Tamko la Sheria ya Kiislamu ya mwaka 1964 na kuhitimishwa na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971”. Alisema, “Jambo la msingi hapa ni kuwa kesi hizo zinahukumiwa na mahakimu wasio na elimu, wala ujio.

Post a Comment

 
Top