Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
KWA UFUPI
- Nukuu: “ Huyu jamaa amekuwa akifanya ziara za mara kwa mara na kujipitisha lango la Ikulu na watu wakimwona wanajua ni mtumishi wa Ikulu na watu amekuwa akiwatapeli”Kamishna Kova
Dar es Salaam. Jeshi
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limemtia nguvuni mkazi mmoja
wa jijini hapa kwa tuhuma za kutumia wadhifa wa Katibu wa Rais Jakaya
Kikwete kujipatia fedha kutoka taasisi na watu binafsi.
Kamishna wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleiman Kova akizungumza na waandishi
wa habari jana alisema, mtu huyo alikuwa akijiita Prosper Mbena ambaye
ndiye Katibu wa Rais Kikwete.
“Mkazi huyo wa Mbagala Rangi Tatu jijini Dar es Salaam tulimkamata jana
(juzi) ambaye amekuwa akijiita Prosper Mbena na ameshatapeli Wizara ya
Ardhi, Maji, taasisi na watu mbalimbali na mara ya mwisho alikamatwa
akichukua Sh300,000,” alisema Kamishna Kova.
Aliongeza: “Tunawaomba wananchi kuwa makini na watu wa aina hii lakini
taasisi zihakikishe wanaweka ulinzi katika milango yao ya kuingilia
pindi wanapomwona mtu anapita pita mara kwa mara wamchukulie hatua na
kujua anachokifanya hapo.”
Kamishana huyo alisema, vitendo vya watu kutumia majina ya watu
kujipatia manufaa hususan ya kifedha, yamekuwapo na ili kuyaondosha
kabisa ni lazima ushiriki wa wananchi na Jeshi la Polisi uwapo kwa
kubadilishana taarifa.
“Tulipata taarifa kutoka kwa mmoja wa waliotaka kutapeliwa na mtego
aliowekewa ni kuambiwa kuwa kati ya zile fedha Sh300,000 kuna fedha
zilibaki hivyo aje kumalizia na hapo hapo tukamweka chini ya ulinzi,”
alisema Kova.
“Vitu vya mwisho au vya kumalizia siyo vizuri, ukichukua umechukua
ukirudi matokeo yake ndiyo hayo yaliyomfika huyu bwana ambaye hana kazi
wala biashara yeyote.”
Tukio hilo siyo la kwanza kutokea kwani yamekuwapo matukio kama haya ya watu kutumia majina ya viongozi kujinufaisha.
Post a Comment