Dar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amesema, ofisi yake haina chama kikubwa na kidogo na kwamba inahudumia vyama vyote vilivyosajiliwa kwa hadhi inayofanana.
Akizungumza juzi, Jaji Mutungi alisema ofisi yake
inavitambua vyama 22 na itatoa huduma zinazofanana kwa hadhi sawa ya
ulezi wa vyama.
Kauli ya Jaji Mutungi imekuja huku mgogoro wa
Chama cha Siasa cha ACT-Tanzania ukifika katika ofisi yake kutafuta
suluhu baada ya viongozi wake wa muda kutofautiana.
“Vyama vyote (mpaka sasa vipo 22 vyenye usajili wa
kudumu)...hakuna chama kidogo au kikubwa kwangu na hii dhana sijui ya
chama kikubwa imetokea wapi, hii haipo kwangu.”
Utashi wa nchi
Kwa upande mwingine, Jaji Mutungi amewataka
wanasiasa kuweka mbele utashi wa kisiasa wakati wa kutekeleza majukumu
yao ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara ndani ya vyama vyao.
Mlezi huyo wa vyama vya siasa alisema,
“Kinachotakiwa ni vyama kujiendesha kama taasisi na siyo mtu, chama
kikiwa kama taasisi hii migogoro haiwezi kuwapo na mimi tangu nimeingia
hapa sijawahi kupewa shinikizo na mtu yoyote yule ili nikipendelee chama
fulani.”
Akizungumzia mgogoro uliopo wa ACT-Tanzania, Jaji
Mtungi alisema baada ya kusikiliza pande zote mbili zinazosigana
alisema, “Nahitaji kupata muda, weledi na umakini katika kufanya
uamuzi...Sitaki kukurupuka baadaye nionekane labda napendelea mtu
fulani.” ACT kimekuwa katika misigano baada ya viongozi wake wa muda
kutofautiana katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho iliyokutana
mwezi uliopita, kumvua uongozi Mwenyekiti wake wa muda, Kadawi Limbu
kwa tuhuma za kukiuka Katiba na kanuni ya chama hicho.
Wengine waliovuliwa uongozi ni Naibu Katibu Mkuu (Bara), Leopold Mahona na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana, Grayson Nyakarungu.
Uamuzi huo pia uliwavua uanachama Richard Mwigamba na mshauri wa chama, Profesa Kitila Mkumbo.
Limbu
Mwenyekiti wa muda wa ACT-Tanzania, Kawawi Limbu
alisema anachofahamu yeye hakuna uchaguzi unaoendelea ndani ya chama
hicho kwa sasa. “Suala letu lipo kwa msajili na ukweli utadhihirika
lakini mimi bado ni mwenyekiti,” alisema Limbu.
“Tulianzisha chama hiki kama wahanga wa demokrasia, mimi
nilitoka CUF kwa sababu kama hizo, Migamba na Kitila walitoka Chadema
wote sisi ni wahanga lakini wao wameshindwa kutekeleza kanuni na sheria
za chama na kufanya wanaoyaona wao.”
“Kama kweli wanajiamini basi hakuna haja ya
kupapalika, wasubiri msajili amalize kazi yake na tuingie katika
uchaguzi waone sasa lakini kama wataendelea utafika wakati tutauzuia
kama ni mahakamani na hili kama wataendelea kukaidi,” anasema Limbu
Mwigamba
Akizungumzia ratiba mbalimbali za chama hicho,
Mwigamba alisema, “msajili hakutuzuia kuendelea na ratiba mbalimbali za
chama ikiwamo za uchaguzi wa ndani bali alituzuia kutozungumzia mgogoro
wetu katika vyombo vya habari.”
Aliongeza, “Kikao cha Halmashauri Kuu ilipitisha
mapendekezo ya Kikao cha Kamati Kuu ya kuanza kwa uchaguzi wa ndani na
ratiba hiyo inaendelea na hakuna mabadiliko yoyote.”
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, uchaguzi ngazi ya shina
ulianza Januari 19 hadi 24 mwaka huu, Tawi Januari 25 hadi 31 mwaka
huu, Kata/Wadi ni Februari mosi hadi 10 mwaka huu, Jimbo Februari 11
hadi 22 mwaka huu na mkoa ni Februari 23 hadi28 mwaka huu.
Ratiba hiyo ilieleza kwamba ngazi ya taifa utaanza
Machi 7 mwaka huu kwa Ngome ya Wazee kuchaguana, Machi 14 mwaka huu
Ngome ya Wanawake, Machi 21 mwaka huu Ngome ya Vijana na mwisho ni Machi
28 mwaka huu kwa Uchaguzi Mkuu wa Taifa.
Akizungumzia utekelezaji wa ratiba hiyo mpaka sasa
Mwigamba alisema, “Mimi ninachojua uchaguzi unaendelea kama
tulivyopanga kwani tulikubaliana katika mkutano wa Halmashauri Kuu na si
vinginevyo.”
Katibu Mkuu huyo alisema, “malengo ya kuanzishwa
kwa chama hiki ni kutaka kuleta mabadiliko na kusaka suluhu ya matatizo
mbalimbali ya Watanzania ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kwani CCM
imeshindwa kuyatatua kwa miaka zaidi ya 50 sasa.”
Aliongeza: “Natoa wito kwa Watanzania kutoteteleka
kwa lolote katika kipindi hiki, tunawaahidi uongozi uliotukuka katika
kipindi chetu chote...sasa tuna wataalamu wetu ambao wanatuandalia
mpango wa kuhakikisha tunashiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu.”MWANANCHI
Post a Comment