0


Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba.

 
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, amesema ameanza mchakato wa kuonana na Rais Jakaya Kikwete, kuwasilisha kilio na kushauriana naye juu ya nguvu kubwa inayotumiwa na Jeshi la Polisi kuwashambulia na kuwakamata wapinzani.


Kadhalika, amesema mazungumzo hayo yatalenga kuwekwa utaratibu wa Jeshi la Polisi kuvitendea haki vyama vya upinzani kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Prof. Lipumba alisema nguvu kubwa inayotumiwa na polisi dhidi ya vyama vya upinzani, haina lengo jema, bali kukandamiza haki za binadamu na demokrasia.

Alisema kwamba ameshaanza hatua za kuomba kuonana na Rais Kikwete na tayari amefika mbali.

Hata hivyo, jana NIPASHE lilipomtafuta Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salvatory Rweyemamu, kueleza kama Rais amepokea maombi ya Prof. Lipumba, hakupatikana na hata ujumbe mfupi wa maneno (sms) aliotumiwa kwenye simu yake ya mkononi, hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.

“Tunataka vyama vyote vitendewe haki na usawa mbele ya nguvu ya dola na siyo kukandamiza upande mmoja, hali hii ikiruhusiwa kuendelea na mwaka huu wa uchaguzi, ni wazi kuwa nchi itaingia katika machafuko,” alisema na kuongeza:

“Vijana wa sasa siyo wa mwaka 2001, Polisi wasifikiri kuwa vijana na wananchi wataendelea kunyamaza na siku wakiamua kulipiza, hakika hakuna atakayepona…nawaomba wananchi wasilipize kisasi kwa askari wanaoishi nao uraiani.”

Alisema kwa tukio la Januari 27, mwaka huu, linaonyesha kuwa Jeshi la Polisi linahitaji marekebisho makubwa ili wafanye kazi kwa weledi kwa kuwa mashambulizi ya mara kwa mara yanajenga kutoaminiana.

ADAI POLISI KUWAPORA
Alisema katika mashambulizi hayo, wafuasi wa CUF waliporwa mali zao na Polisi ikiwamo kamera ya picha za mnato na video ya Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Abdul Kambaya, na mwaka 2001 walipora saa yake ambayo haijarejeshwa hadi sasa.

Alisema baada ya kuwakamata walengwa, waliwasikia polisi wakisema wanapiga mabomu na risasi hewani za kuwaaga wananchi, jambo alilolieleza kuwa ni la kustajaabisha.

Prof. Lipumba alisema katika barua ya polisi iliyowasilishwa Januari 27, mwaka huu, ilieleza kuwa kama hawajaridhika na maamuzi ya kuzuia maandamano na mkutano wa hadhara, wakate rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani bila kuwapo muda wa kufanya hivyo.

Aidha, alisema ni kitendo cha fedheha na aibu kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, kusema uongo ndani ya Bunge kuwa barua ya polisi ilipelekwa CUF saa kadhaa kabla na inaonekana suala hilo Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, alikuwa analijua kwa kuwa alipewa nakala. CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

 
Top