0

 
             Vijana wakiwania kufukuza upepo

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama amesema michuano ya kimataifa ya Kilimanjaro Marathon inasaidia kunyanyua uchumi wa mkoa huo uliopo Kaskazini mwa Tanzania kwa watalii wengi kushiriki.
Gama amesema katika taarifa yake kuwa kuwa wakazi wengi wanapata ajira wakati wa mbio na mahoteli kujaa wageni kutokana na kufurika wakimbiaji wa kimataifa.
Zaidi ya wakimbiaji 800 kutoka nchi 40 zikiwemo za America na Uingereza wanategemewa kushiriki mbio hizo zitakazofanyika March 1 mjini Moshi, mkoa wa Kilimanjaro Kaskazini mwa Tanzania.
Mbio hizo hufanyika kila mwaka na zinatambulika na shirikisho la riadha duniani, IAAF.Kwa mujibu wa John Addison, mmoja wa waandaaji kutoka kampuni ya Wild Frontiers, wakimbiaji wengi wa kimataifa wameonesha nia ya kushiriki.
Miongoni mwa malengo ya mbio hizo, mbali ya kuwaandaa washiriki na mashindano makubwa ya kimataifa, ni kuendeleza utalii ambapo wakimbiaji wengi wa kimataifa hupata fursa ya kuuona mlima Kilimanjaro, ambao ni mrefu kuliko milima yote barani Afrika.
Nchi ambazo zinategemewa kushiriki, mbali na America na Uingereza ni pamoja na Canada, Japan, Uganda, Zimbabwe na Kenya.
Nyingine ni Sweden, Australia, Hungary, Germany, Sweden, Norway, Italy, France, Japan, China, Zambia, Morocco, Swaziland, Nigeria na Malawi, ambapo washiriki huthibitisha kupitia mtandao.
Washiriki watashindana katika mbio ndefu (marathon-kilometa 42.2) na nusu marathon (kilometa 21.1).
Washiriki pia watashiriki katika mbio mbalimbali kama vile za kilometa 5 kwa ajili ya afya.
Kenya, miongoni mwa nchi mashuhuri katika riadha barani Afrika, imekuwa ikitawala katika mbio ndefu na kushinda medali pamoja na fedha kutoka kwa waandaaji na wadhamini. Mbio hizo zimetimiza miaka 13 tangu kuanzishwa kwake.
David Rutoh kutoka Kenya alishinda marathon ya mwaka jana kwa upande wa wanaume akimaliza mbio katika muda wa 2:16:06 wakati Fridah Lodepa (Kenya) alishinda kwa upande wa wanawake akitumia muda wa 2:40:26.

Post a Comment

 
Top