MAAZIMIO YA KAMATI KUU YA CCM -:
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Jana tarehe
13/01/2015 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa chini ya uongozi
wa Mwenyekiti wake wa Taifa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete ilifanya kikao
chake cha kawaida cha siku moja Kisiwandui Mjini Zanzibar.
Pamoja na mambo mengine baadhi ya mambo yaliyojadiliwa na Kamati Kuu ni pamoja na:-
1. SAKATA LA AKAUNTI YA ESCROW.
Chama Cha
Mapinduzi kimesikitishwa sana na sakata hili. Baada ya kulijadili kwa
muda mrefu na kwa kina Kamati Kuu imeamua yafuatayo:-,
i). Pamoja
na yale ambayo yameshatekelezwa na serikali, Kamati Kuu imeitaka
serikali na vyombo vinavyohusika kuendelea kutekeleza maazimio ya bunge
juu ya swala hilo.
ii). Kamati
Kuu imewataka wote wanaopewa dhamana wajenge utamaduni wa kuwajibika kwa
dhamana zao, na wasipowajibika waliowapa dhamana wachukue hatua za
kuwawajibisha.
iii). Aidha
Kamati Kuu imeiagiza Kamati Ndogo ya Maadili kuchukua hatua za kimaadili
kwa wale wote waliohusika na ukiukwaji wa maadili kwenye sakata la Escrow
na wako kwenye vikao vya maamuzi vya Chama. Kikao cha Kamati Ndogo ya
Maadili kitafanyika tarehe 19/01/2015 kwa ajili ya utekelezaji wa agizo
hilo.
2. WALIOPEWA ADHABU KWA KUKIUKA MAADILI YA CHAMA.
Itakumbukwa
kuna makada sita wa CCM walipewa adhabu kwa kuhusishwa na ukiukwaji wa
maadili kwenye mchakato wa kutaka kuteuliwa na CCM kugombea urais,
watamaliza muda wa adhabu zao mwezi wa pili mwaka 2015.
Baada ya
muda wa adhabu zao kuisha, itafanyika tathimini kuona kama walizingatia
mashariti ya adhabu zao. Na kama kuna ambao watakutwa hawakuzingatia
mashariti ya adhabu zao wataongezewa adhabu.
3. SOKO LA MAHINDI.
Kamati Kuu
imepokea taarifa ya mwenendo wa soko la mahindi nchini. Baada ya
tathimini na uchambuzi, pamoja na kazi iliyofanywa na serikali, Kamati
Kuu imeiagiza serikali kuangalia upya mfumo unaotumiwa na Hifadhi ya
Taifa ya Chakula ( NFRA)katika ununuzi wa mahindi, ili unufaishe zaidi
wakulima badala ya utaratibu wa sasa ambao kwa kiasi kikubwa unanufaisha
zaidi mawakala badala ya wakulima moja kwa moja.
4. RATIBA YA VIKAO VYA CHAMA.
Kamati Kuu
imepitisha ratiba ya shughuli mbalimbali za Chama kwa mwaka 2015.Aidha
ratiba ya mchakato wa kuwapata wagombea wa CCM ndani ya dola utapangwa
na vikao vijavyo vya Chama.
Nape Moses Nnauye
CCM Secretary for Ideology & Publicity.
Post a Comment