0

Maofisa wa Wanyamapori wakishirikiana na polisi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), wakipekua sanduku lililobeba kenge ambalo lilikamatwa kwa mmoja wa abiria jijini Dar es Salaam jana.
Raia wa Kuwait, Hussain Ahmed Ally Mansour (34), amekamatwa na maofisa usalama na Jeshi la Polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa tuhuma za kutaka kusafirisha kenge hai 149 wenye thamani ya Sh. milioni 6.33 kwenda nchini Kuwait.

Tukio hilo la kusafirisha wanyama hai ni la pili kutokea nchini, la kwanza lilitokea mwaka 2010, baada ya twiga hai wanne waliosafirishwa kwenda nje katika mazingira yenye utata na hivyo kuzua mjadala ndani na nje ya nchi.

Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege Tanzania, Hamis Seleman, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi saa 5:20 usiku akiwa ameficha kenge hao kwenye mifuko midogo 15 ndani ya begi jeusi kwa lengo la kuwasafirisha kwenda Kuwait kupitia Dubai kwa ndege ya Shirika la Emirates.

Alisema mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa na hati ya kusafiria yenye namba  003870237, alibainika akitaka kusafirisha kenge hao baada ya vyombo vya usalama katika uwanja huo kufanya upekuzi wa mizigo kabla ya abiria kuruhusiwa kuingia kwenye ndege.

Kamanda Seleman alisema baada ya kukamatwa, mtuhumiwa huyo alifikishwa katika Kituo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege Dar es Salaam kwa ajili kuhojiwa ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Aliongeza kuwa baada ya kupekua, walibaini kuwa kenge 15 walikuwa wamekufa kutokana na kukosa chakula.

“Tukio hili linatushangaza kwa sababu mtuhumiwa aliingia nchini Januari 6, mwaka huu na Januari 7, mwaka huu alikuwa anataka kuondoka kurejea kwao nchini Kuwait. Tunajiuliza; alipata muda wapi kukusanya kenge wote hawa kwa muda mfupi?” alihoji Kamanda Seleman.

Alisema mazingira ya tukio hilo yanaonyesha dalili kuwa baadhi ya watu wasiokuwa na uzalendo kwa  wanyama na viumbe hai, walimsaidia kufanikisha hujuma hiyo.

Kamanda Seleman alisema suala la kupambana na ujangili wa wanyama na viumbe hai siyo kazi ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Jeshi la Polisi pekee, bali operesheni hiyo inatakiwa kutekelezwa na Watanzania wote.

Alisema kenge hao wamekabidhiwa kwa Idara ya Maliasili na Utalii ambao watakuwa na jukumu la kuwahifadhi.

Katika tukio la kusafirisha wanyama hai lililotokea Novemba 26, mwaka 2010, raia wa Pakistan, Kamran Ahmed, alikamatwa kwa kuwatorosha wanyama hai 153 wakiwamo twiga wanne, kwenda Doha, Qatar kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa kutumia ndege ya kijeshi, namba C17.

Kwa mujibu kifungu namba 84(1) cha Sheria namba 5 ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2009, kitendo cha kusafirisha wanyama hao ni kinyume cha sheria ya nchi.

Wanyama hai waliodaiwa kutoroshwa walikuwa twiga wanne, chui, ndege wa aina mbalimbali, duma, nyati, pofu, punda milia na swala bila leseni na kinyume cha taratibu.

Mahakama  ya Hakimu Mkazi Moshi, mkoani Kilimanjaro, mwezi uliopita, ilimhukumu kifungo cha miaka 60 jela mshtakiwa katika kesi ya utoroshaji wa wanyama hai 153, na kuwaachia huru Watanzania watatu.

Katika hukumu hiyo, Kamran alikutwa na makosa manne, kushiriki na kula njama ya kutenda uhalifu kinyume na  kifungu cha 57 (1), sehemu ya 4(1), sura ya kwanza ya kosa la uhujumu uchumi na kushiriki utoroshaji wa wanyama hai wenye thamani ya Sh. 170,575,500.

Kosa la nne kuisababishia serikali hasara ya Dola 113.7 kwa kufanya biashara kinyume cha sheria.

KAULI YA SERIKALI
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akizungumza na NIPASHE jana, alisema tukio la kukamatwa kwa kenge JNIA litakuwa ni fundisho kwa wengine ambao wanadhani operesheni ya kudhibiti wanyama na viumbe hai ni mchezo.

“Napenda kutoa onyo kwa watu wote kuacha tabia hiyo kwa kuwa tumeweka mtandano kila kona ya nchi kwa ajili ya kubaini watakaofanya uhalifu wa aina hiyo,” alisema.

Waziri Nyalandu alisema Serikali itaendelea kupambana na kudhibiti matukio hayo, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua kali za kisheria watakaopatikana na hatia.


 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

 
Top