0
Anasema hali hiyo si nzuri na inatoa changamoto mpya katika vita dhidi ya rushwa hasa kutokana na wananchi wengi kupoteza imani katika vita hiyo, kwa kuwa ndiyo wanaoathirika moja kwa moja na hawaoni hatua zozote madhubuti kukomesha na kuwashughulikia watuhumiwa wa matukio hayo.
“Kwa viwango hivyo vya kimataifa, Watanzania wamekuwa wakitoa mara chache chini ya wastani wa kimataifa katika masuala yanayohusiana na ardhi kwa asilimia 10 ikilinganishwa na wastani wa kimataifa wa asilimia 21 na asilimia tano katika elimu ambayo ni chini ya wastani wa kimataifa wa asilimia 16,” inaeleza ripoti hiyo.
Uthibitisho huo unadhihirisha namna ambavyo Watanzania wamekuwa wakisumbuliwa na kulazimishwa kutoa rushwa wanapopata matatizo yanayohitaji huduma ya taasisi hiyo muhimu ya usalama kwa umma ambayo inaendeshwa na Serikali kwa asilimia 100.
Mushi anasema Watanzania pia wamekuwa wakiingia katika mtego wa kutoa rushwa baada ya kutembelea ofisi za Serikali au watoa huduma katika sekta binafsi kama kamati za maji za vijiji, mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika ya dini au shule zilizo katika maeneo yao.
Katika mahojiano ya utafiti huo, idadi kubwa ya wananchi walisema waliwahi kuombwa rushwa na watu watatu kati ya watano, sawa na asilimia 60 waliombwa rushwa na polisi na mmoja kati ya watatu (asilimia 34) waliombwa rushwa walipokuwa wakitafuta kazi.
Katika mahojiano zaidi kuhusu mara ngapi waliwahi kuombwa rushwa, walisema polisi ndio wanaoongoza kwa kuomba rushwa na asilimia 41 walitoa kwa kuambiwa na asilimia mbili walitoa bila kuambiwa.
“Tatizo kubwa hapa ni kwamba wananchi wamepoteza imani kabisa kwa sababu hata zile kesi kubwa za rushwa zinazoibuliwa, mara nyingi zimekuwa zikipotelea hewani na hakuna anayewajibishwa,” anasema Mushi na kuongeza:
“Hata Takukuru iliyopewa jukumu la kuchunguza haijapewa meno ya kutosha.
Wananchi walisema wazi kwamba wanapenda kuiona taasisi hiyo ikiwa na uwezo wa kusimamia uchunguzi na hata kuendesha kesi hizo yenyewe, yaani iwe na uwezo wa kufuatilia mwanzo hadi kutoa uamuzi wa mwisho.”
Kwa kutumia utafiti wa kipimo cha rushwa duniani wa 2013, uliofanywa na shirika la Transparency International, Watanzania wamekuwa wakilipa hongo mara nyingi zaidi kwa maofisa wa polisi kuliko wastani wa kimataifa ambao ni asilimia 34.
Uelewa wa wananchi kuhusu rushwa kubwa
Hata hivyo, wakati rushwa ikishtadi nchini, Watanzania wengi hawana taarifa za kutosha na wengi zaidi hawajui kabisa kuhusu kashfa kubwa za rushwa zinazoelezwa katika vyombo vya habari.
Hili ni suala gumu lililoguswa katika ripoti ya utafiti huo na hadi matokeo yanatoka, asilimia zaidi ya 78 haikujua lolote kuhusu kashfa ya IPTL, asilimia 74 haijui lolote kuhusu kashfa ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Nishati, David Jairo na asilimia 67 hawajui lolote kuhusu kashfa ya ununuzi wa rada.
Wengine ni asilimia 52 ambao hawajui lolote kuhusu kashfa ya EPA na zaidi ya asilimia 44 ambao hawajui lolote kuhusu kashfa ya Richmond.
Wastani huo unashtua kwa sababu kwa idadi hiyo kubwa ya Watanzania wasiojua lolote kuhusu kashfa hizo kubwa za rushwa zinazowagusa moja kwa moja viongozi waandamizi serikalini, zimekuwa zikiripotiwa katika vyombo vya habari na kujadiliwa kwa kina bungeni na kisha umma wa Watanzania.
Kwa wastani, matatizo mengi ya nchi yanapata ukakasi katika kuyatatua hasa kashfa za rushwa kwa kuwa uelewa wa wananchi uko chini, licha ya kutangazwa na vyombo vya habari na kutawala mijadala ya kisiasa.
Katika utafiti huo, suala la rushwa katika sekta za usalama, siasa, kodi, ardhi, afya, elimu, maji, Serikali za Mitaa, mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika ya dini inawagusa zaidi ya asilimia 50 ambao wamefikia hatua ya kuiona kama ni kitu cha kawaida.
“Wengi wamekuwa wakitoa rushwa wakiwa kwenye hali tete, hasa wanapokutana na polisi au wanapohitaji huduma za uhakika za afya na miongoni mwa wahojiwa watatu kati ya watano waliripoti kwamba walishinikizwa kutoa rushwa walipokutana na polisi mara ya mwisho,” inaeleza ripoti.
Uombaji rushwa unaoshika nafasi ya pili ni ule unaowakabili wananchi wanapoomba ajira na sasa rushwa inatazamwa kama kitu cha kawaida kabisa au cha kawaida kiasi kwenye huduma zote za Serikali isipokuwa katika sekta ya maji pekee.
Udhibiti wa rushwa
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wakati wafadhili, wanasiasa na mashirika yasiyo ya kiserikali yakijikita kupambana na kashfa kubwa za rushwa, wananchi wengi wanaangalia zaidi aina ya rushwa inayowagusa moja kwa moja na kuathiri maisha yao ya kila siku.
Tatizo linaloonekana kuwa na athari ya moja kwa moja ni namna tabaka la wasomi na wanasiasa wanavyoelekeza nguvu zao katika rushwa wanazoziita kubwa na kutotilia maanani rushwa wanazoziita ndogo ambazo ndizo zinazowagusa wananchi moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku katika huduma za polisi, afya, elimu na ardhi.MWANANCHI

Post a Comment

 
Top