Bei ya korosho ghafi katika soko la minada chini ya
mfumo wa stakabadhi ghalani imeimairika na kufikia Sh1,660 kutoka
Sh1,500 kwa kilo katika wiki mbili zilizopita.
Akizungumza jana ofisini kwake, Mkurugenzi Mkuu wa
Bodi ya Korosho nchini (CBT), Mfaume Juma amesema, mwenendo wa bei
katika minada ya Novemba 17 hadi 30 umeonyesha kupanda.
“Tofauti na minada ya awali, bei ilionyesha
kushuka kwa kufikia Sh1,500 kwa kilo, hizi wiki mbili bei imepanda ”
alisema Juma na kuongeza;
“Kuimarika kwa bei kunatokana na wanunuzi kubaini
uhakika wa ubora wa korosho zinazopitia mfumo wa stakabadhi
ghalani...pia kutekelezwa kwa makubaliano ya matumizi rafiki ya bandari
ya Mtwara, meli za kubeba korosho zimeshaanza kuwasili.”
Alisema jumla ya tani 139,123.77 za korosho ghafi
zimekusanywa ikiwa ni ongezeko la tani 9,000 la korosho zilizokusanywa
katika msimu uliopita hali inayoashiria kuongezeka kwa uzalishaji wa zao
hilo.
“Msimu 2013/14 tulikusanya jumla ya tani
130,123.77 kiasi hiki kimeongezeka katika msimu huu na hadi sasa
tumekusanya tani 139,123.77...bado wakulima wanazo korosho na ukusanyaji
unaendelea hii ni dalili njema kwetu.”
Mkurugenzi huyo alisema pamoja na mafanikio hayo
changamoto inayowakabili wakulima ni kulinda ubora wa korosho zao wakati
wa kuhifadhi.
“Katika wiki mbili zilizopita tumebaini kupungua
kidogo kwa ubora wa korosho kunakosababishwa na baadhi ya wakulima
kuweka korosho katika viroba kabla ya kuzipeleka kwenye vyama vya msingi
...viroba vinatunza joto, korosho zinapoteza unyevu ni vyema
wakahifadhi kwenye magunia.” ya katani au juti” alisisistiza Juma.MWANANCHI
Post a Comment