0

Baadhi ya wananchi mkoani Ruvuma wamesema wanakosa imani na baadhi ya wawakilishi wao bungeni kwa kuonyesha nia ya wazi ya kutaka kuwatetea watuhumiwa wa fedha za Akaunti ya Escrow.

Msasumbuko Ngonyani na Thadei Njajule, walisema awali wabunge walionyesha kuweka kando itikadi na ushabiki wa vyama vyao na kuonyesha msimamo wa pamoja wa kukerwa na ubadhirifu huo.

Walisema kitendo cha baadhi ya wabunge kuwa na kauli kinzani kuhusiana na suala hilo nyeti ambalo linaligawa taifa, kinawafanya wananchi kukosa imani na wawakilishi wao bungeni pamoja na serikali kwa ujumla kwa sababu matukio hayo ya wizi na ubadhirifu yameibuliwa na wabunge wenyewe na wananchi hawakuyajua kabla.

Walisema baadhi ya wakulima wa mahindi mkoani Ruvuma ambao walizalisha mahindi kwa kiasi kikubwa na gharama kubwa mpaka leo mashindi yao hayajanunuliwa na yameanza kuharibika kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha lakini kikundi kidogo cha viongozi kinatajwa kuchukua mabilioni ya fedha na baadhi ya wabunge wanaonesha kukitetea kikundi hicho.

Aidha NIPASHE imeshuhudia mikusanyiko ya watu wakifuatilia kinachoendelea bungeni huku baadhi wakishauri wahusika wawajibike au mamlaka husika zichukue hatua za haraka na makusudi kuwawajibisha kama ilivyotokea kwa baadhi ya watuhumiwa ambao hawakuwa tayari kuwajibika.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

 
Top