Doha, Qatar. Waziri Mkuu Mizengo Pinda anaendelea na ziara yake ya siku tatu nchini Qatar na kazi kubwa ni kutafuta wawekezaji katika sekta ya mafuta na gesi pamoja na maeneo mengine ya kiuchumi ikiwemo utalii na fursa za biashara.
Awali Waziri Mkuu alikuwa na ziara kama hiyo
nchini Dubai kabla ya kukatisha ziara hiyo Alhamisi iliyopita baada ya
kuitwa na Rais Jakaya Kikwete kwa shughuli maalumu.
Katika ziara hiyo hapa Qatar, Waziri Mkuu
alipokewa kwa gwaride la heshima, atafanya mazungumzo na mawaziri
watano; Naibu Waziri wa Nishati na suala kubwa linalotarajiwa
kuzungumzwa ni kuhusu uvumbuzi wa mafuta na gesi.
Akiwa Dubai, Waziri Mkuu alikutana na maofisa
watendaji wakuu wa Emirates National Oil Company (ENOC), Said Foemy na
Fandraj Govindaraj kuzungumzia suala la uwekezaji katika sekta ya mafuta
na gesi.
Mawaziri wengine anaotarajia kukutana nao ni;
Waziri wa Masuala ya Uchumi, Waziri wa Vitegauchumi, Waziri wa
Miundombinu na Usafirishaji na Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Jamii.
Ratiba ya ziara hiyo iliyotolewa jana jioni
inaonyesha, Waziri Mkuu kabla ya kukutana na mawaziri hao, leo Jumapili
atakuwa na mazungumzo na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Serikali ya
Qatar, Sheikh Abdullah Nasser Al Thani.
Baada ya mazungumzo hayo, Waziri Mkuu na ujumbe
wake, watapata chakula cha mchana na Waziri Mkuu huyo kabla ya kukutana
na Watanzania wanaoishi Qatar baadaye jioni.
Ratiba inaonyesha kuwa kesho Jumatatu, Waziri Mkuu
atatembelea Bandari ya Qatar na kufanya mazungumzo na maofisa wa
bandari hiyo na baadaye mchana atakuwa na mazungumzo na Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Qatar, Jassim Bin Khalifa Bin Ali Thani
pamoja na wanachama na wanajumuiya hiyo.
Waziri Mkuu pamoja na ujumbe wake, wanatarajia kurejea nchini Jumanne baada ya ziara hiyo ya siku tatu.MWANANCHI
Post a Comment