0
 
Dar es Salaam. Tanzania inaadhimisha miaka 53 ya Uhuru leo huku wananchi wa kada mbalimbali wakiielezea siku hii kuwa haina uhalisia wa maisha ya Watanzania.
Rais Jakaya Kikwete atakuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo itakayofanyika katika Uwanja wa Taifa, ambako atakagua gwaride la vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama na baadaye kuwatunuku nishani za heshima kwa watu mbalimbali waliotumikia Taifa.
Katika maadhimisho hayo, pia kutakuwa na michezo ya halaiki, sarakasi, ngoma za asili kutoka katika baadhi ya mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar. Kaulimbiu ya mwaka huu ni; “Miaka 53 ya uhuru; ingia katika historia ya nchi yetu; jitokeze kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa.”
Wakati hayo yakifanyika, wadau mbalimbali wameielezea miaka 53 ya Uhuru kwa mtazamo tofauti.
Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambacho pia kinatimiza miaka 53 leo, Profesa Shadrack Mwakalila alisema sherehe hizo zinafanyika wakati nchi inatajwa kukithiri kwa vitendo vya ukosefu wa maadili kwa viongozi.
Alisema hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa mafunzo na elimu ya maadili kwa viongozi kama ilivyokuwa siku zilizopita, hivyo kuna haja ya mafunzo hayo kurudishwa.
Alisema miaka ya 1971 hadi 1991 wakati chuo hicho kikiitwa Chuo cha Chama Kivukoni, kilikuwa kinatoa mafunzo ya maadili na uongozi kwa watendaji wote wa Serikali kabla hawajaenda kulitumikia Taifa, hali ambayo sasa haipo na ndiyo inayochangia kinachotokea sasa.
Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha, alisema tofauti na mwaka 1972 hadi 1980 wakati elimu iliyokuwa inatolewa ilikuwa na mwelekeo, kwa sasa kiwango kimeshuka kwa kiasi kikubwa.
Alisema kuna sababu mbalimbali za kushuka, ikiwamo ukosefu wa walimu, motisha kwa walimu na zana za kufundishia.
Profesa Mpangala alisema pamoja na sasa kuwapo vyuo vingi, tatizo kubwa ni ukosefu wa ajira... “Kila mwaka vyuo vinamwaga wahitimu, lakini hawana kazi. Uchumi wa Tanzania hauwezi kuwaandaa wasomi kuingia kwenye soko la ushindani… tatizo siasa zinaingizwa kwenye elimu,” alisema.
Mtaalamu wa maendeleo na siasa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Idd Makombe alisema miaka 53 ni mingi na kama nchi ilitakiwa kuwa imepiga hatua zaidi kimaendeleo badala ya kuendelea kuwa maskini duniani.
Alisema kuna nchi ambazo kipindi Tanzania inapata uhuru zilikuwa sawa nayo lakini leo zimepiga hatua.
“Ili kufikia malengo yanayoendana na miaka 53, tunahitaji kuwa na viongozi wazalendo... tufanye kitu cha watu wote kiwe cha watu wote, kwa sasa hili halipo.”
Mkurugenzi wa Sera wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Hussein Kamote alisema sekta ya viwanda bado ina safari ndefu ya kufikia Malengo ya Milenia 2025 ya kuwa na Pato la Taifa (GDP) linalotokana na viwanda kuwa asilimia 15.
Alisema miaka 53 iliyopita, mchango wa sekta hiyo katika GDP ulikuwa asilimia mbili, kwa sasa umefikia asilimia tisa lakini bado kuna changamoto ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi.
Alisema Taifa likihakikisha umeme unapatikana wa kutosha na wa bei nafuu, reli na bandari zikaimarishwa, tunaweza kupiga hatua zaidi... “Lakini vyuo vitoe wanafunzi watakaokwenda kushindana katika soko la ajira kwenye viwanda, ili miaka 10 au 15 ijayo tuweze kuona matokeo chanya ya sekta ya viwanda.”
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Repoa, Profesa Samuel Wangwe alisema kwa kipindi chote matatizo kama umaskini, ujinga na maradhi ambayo yalitajwa kama maadui wa Taifa, hayajaisha na kubakia kama changamoto zinazotakiwa kutatuliwa.
“Umaskini bado ni changamoto kubwa inayohitaji kufanyiwa mageuzi, kilimo kiwezeshwe ili kiwasaidie Watanzania kuepukana na maskini... maradhi na ujinga kwa kiasi fulani vimepiga hatua kwa kipindi hiki cha miaka 53,” alisema Profesa Wangwe.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga alisema sherehe za miaka 53 ya Uhuru zingependeza kama kungekuwa na sheria ya kupata habari.
“Ingependeza kama tungekuwa na sheria ya habari, lakini leo tunahuzunika kwa kukosa sheria hiyo ambayo ilikuwa ifikishwe bungeni Aprili, mwaka huu lakini sasa itapelekwa Februari mwakani,” alisema Mukajanga na kuongeza:
“Tuna masikitiko, tunaposherehekea miaka 53 bado tuna sheria mbovu za kukandamiza uhuru wa habari ambazo hazijaondolewa, ingawa, jambo pekee la kujivunia ni Katiba Inayopendekezwa imetaja uhuru wa vyombo vya habari tofauti na Katiba ya sasa kubainisha haki ya kupata habari kwa ujumla jumla... hatujui kama itapita au la, lakini imependekeza hilo.”MWANANCHI

Post a Comment

 
Top