0
http://freemedia.co.tz/daima/wp-content/uploads/2014/11/mayai.jpgAFYA za wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ziko hatarini kutokana na kudaiwa kula mayai ya kuku mabovu ambayo yameingizwa nchini kinyemela na baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa ni wawekezaji.

Akizungumza na Tanzania Daima jijini jana kwa masharti ya kutotajwa jina, mmoja wa madaktari wa mifugo, alisema mayai hayo yamekuwa yakisambazwa mitaani kwa wingi kila siku.

Alisema kama Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi itashindwa kuwadhibiti wakezaji hao wasio waminifu wakaingiza mayai hayo kinyume na sheria, basi serikali ijiandae kwa fedha nyingi kwa ajili ya kuja kutibu magojwa yatakayotokana na ulaji wa mayai hayo.

“Nimejaribu kupita katika maeneo yanakouzwa kwa kweli hali ni mbaya, kwani ni uozo mtupu kiasi kwamba hata wakazi wanaoishi karibu na maduka hayo kiafya wako mashakani na wanashangaa kuona mayai hayo yakiachwa bila kudhibitiwa,” alisema daktari huyo.

Alizitaja majina baadhi ya kampuni (zinahifadhiwa kwa sasa), zinazohusika na uingizaji wa mayai hayo, huku zikidaiwa pia kuwa na mashine za kutengenezea mayai bandia katika mashamba yao yaliyoko wilayani Mkuranga mkoani Pwani.

Wakati hali ikiwa hivyo, Tanzania Daima imepata waraka kutoka kwa Ofisa Mfawidhi (ZVC), Kanda ya Mashariki Temeke, ukiomba kupatiwa askari kwa ajili ya zoezi la ukamataji wa mayai na nyama za kuku zinazoingizwa nchini kinyume na sheria, kanuni na taratibu.

Waraka huo umesainiwa na mtu aliyetambulika kwa jina la Dk. Mapouusa A.R.M, kwa niaba ya Ofisa Mfawidhi ZVC wa kanda hiyo.

Waraka huo kumb. Na. VEZ/D6/01/51 ulioandikwa Oktoba 28 mwaka huu, ulikuwa ukiomba kupatiwa askari wanne kwa ajili ya zoezi la kukamata mayai na nyama za kuku zinazoingizwa kutoka nje ya nchi kinyume cha sheria na taratibu za nchi.

Sehemu ya waraka huo, unaonesha kuwa kazi hiyo ya kukamata chakula hicho itakuwa ya mwezi mmoja, ikianzia Oktoba 28 hadi Novemba 28 mwaka huu.

Dk. Mapoussa, alibainisha kufanya hivyo kunatokana na ukweli kwamba, uingizaji huo wa mayai na nyama ni kinyume cha sheria ya magonjwa ya mifugo ya 2003 na kanuni ya mwaka 2007.

“Tunapaswa kuyakamata na kuwapeleka mahakamani wahusika ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema Mapoussa.

Hata hivyo, Tanzania Daima, limebaini mayai hayo bado yanaendelea kuingizwa na kusambazwa katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kwa wingi.TANZANIA DAIMA

Post a Comment

 
Top