Dar es Salaam. Ushirikiano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) siku si nyingi huenda ukatambulika kisheria baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kueleza mpango wake wa kuifanyia maboresho Sheria ya Vyama vya Siasa ili kutambua ushirikiano wa aina hiyo.
Juzi Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Mutungi alieleza ugumu wa Ukawa katika kushughulikia suala la ruzuku,
lakini jana Msaidizi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza
alisema maboresho yanaweza kuondoa mvutano kuhusu suala la ruzuku kwa
vyama vitakavyoamua kushirikiana kwa sababu ushirikiano huo utakuwa wa
kisheria.
Wakati Nyahoza akieleza hayo jana ofisini kwake
jijini Dar es Salaam kwa ruhusa ya Jaji Mutungi, Mwenyekiti Mwenza wa
Ukawa, Freeman Mbowe alisema moja kati ya vitu vinavyofanyiwa kazi na
umoja huo kwa sasa ni kuhakikisha sheria ya vyama vya siasa inaboreshwa,
ili vyama viweze kuungana na kushirikiana.
Hivi karibuni aliyekuwa Msajili wa Vyama vya
Siasa, John Tendwa alisema ili vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni
Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD viweze kuungana Sheria ya Vyama vya
Siasa inatakiwa kurekebishwa ili kuviwezesha kusimamisha mgombea mmoja.
Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, vyama vya siasa
vinaweza kumuunga mkono mgombea wa chama fulani lakini haviwezi kuwa na
umoja utakaopewa jina kisheria, kisha kusimamisha mgombea mmoja lakini
kila chama kikibaki na utambulisho wake na kusisitiza kuwa mabadiliko ya
sheria hiyo aliyaacha ofisini kwake.
Jumapili iliyopita vyama hivyo vinne vilisaini
makubaliano ya kushirikiana katika mambo saba, likiwamo la kusimamisha
mgombea mmoja katika ngazi zote kuanzia chaguzi za serikali za mitaa
hadi Uchaguzi Mkuu ujao.
Katika ufafanuzi wake Nyahoza alisema, “Mchakato
huu unaendelea na uko katika hatua nzuri. Wadau wametoa maoni yao kwamba
ushirikiano wa vyama utambulike kisheria na kupewa usajili na Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa.”
Aliongeza, “Kwa hali ilivyo sasa ushirikiano wa
Ukawa hautambuliki kisheria lakini pia sheria haizuii uwapo wake.
Tunachotaka kukifanya ni kuongeza kipengele cha kutambua ushirikiano wa
vyama katika sheria ya vyama vya siasa.”
Alifafanua kuwa kama kipengele hicho kingekuwapo,
ofisi ya msajili ingetoa usajili wa ushirikiano wa Ukawa huku akitolea
mfano ushirikiano wa vyama vya siasa nchini Kenya.
“Tungekuwa na kipengele hicho katika sheria maana
yake ni kwamba makubaliano ya Ukawa yangesajiliwa na msajili na hicho
ndiyo kilichofanyika Kenya,” alisema.
Nchini Kenya vyama viliungana na kuzaliwa umoja
uliopewa jina la Jubilee na kusimamisha mgombea mmoja na muungano huo
ndio uliotoa mshindi, Rais Uhuru Kenyatta. Pia, viliungana vyama vingine
na kuzaliwa umoja mwingine uliopewa jina la Cord.
“Ushirikiano ukitambulika kisheria vyama
vitashirikiana katika kupata haki za pamoja ikiwa ni pamoja na kufanya
mikutano ya pamoja, hata utaratibu wa ruzuku kupitia ofisi ya msajili
utakuwa mzuri maana yanakuwa ni makubaliano ya kisheria,” alisema.
Alipoulizwa lini muswada huo utawasilishwa bungeni alisema:
“Bado. Hatuwezi kusema lini lakini mchakato upo katika hatua nzuri na
hili tutalifanya siku za karibuni.”
Akizungumzia suala hilo Mbowe alisema, “Jambo hilo
hivi sasa ndio tunalifanyia kazi. Achana na ushirikiano, kama tukitaka
kuungana ni lazima tukubali kupoteza wabunge, madiwani na kila kitu. Ni
lazima tuanze upya. Ndio maana nasema sheria hii ipo kwa ajili ya
kuvifanya vyama vya upinzani visiungane.”
Mbowe alisema hata Katiba ya sasa haisemi chochote
juu ya vyama kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama ilivyo kwa Katiba
ya Zanzibar.
“Tunapenda kuungana lakini tatizo ni sheria, jambo
hili ni zuri na tunaweza kulipigania likapelekwa bungeni lakini
kutokana na wingi wa wabunge wa CCM wanaweza wakalipinga,” alisema.
Tendwa
Tendwa ambaye alistaafu nafasi ya Usajili wa Vyama vya Siasa Agosti mwaka jana, alisema
vyama vinavyounda Ukawa kwa sasa haviwezi kuungana
na kuweka mgombea mmoja wa urais na kumuita mgombea wa Ukawa, kwani
sheria haisemi hivyo.
Alisema mapendekezo ya mabadiliko ya sheria hiyo
aliyaacha ofisini na kwamba yanatakiwa kwenda katika Sekretarieti ya
Baraza la Mawaziri, Kamati za Makatibu Wakuu, Baraza la Mawaziri ambalo
linaweza kutoa maelezo kwenye kamati yake ndogo ambayo inashughulikia
masuala ya kisheria.
Alisema kuwa jambo hilo lilipopendekezwa wadau
waliliunga mkono bila kufahamu kuwa muungano uliopendekezwa sio ule
unaoweza kuvifanya vyama vya siasa kusimamisha mgombea mmoja na kuwa na
jina moja.
Alisema mapendekezo hayo yalikuwa ni mapendekezo ya kuunganisha vyama (Merge) ambayo ni kuunganisha vyama na kuwa chama kimoja.
Alisema mfumo uliotakiwa upendekezwe na wadau ni
muungano wa vyama (Alliance) ambao vyama vinaweza kushirikiana chini ya
mwamvuli mmoja kwa kujiita jina moja, kisha kusimamisha mgombea mmoja
kwa jina hilo, ila kila chama kinabaki na utambulisho wake.
Alisema hivi sasa jambo hilo linatakiwa kupigiwa
debe na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ili lifanyiwe marekebisho na
muungano wa ‘Alliance’ ndio uingie katika sheria.MWANANCHI
Post a Comment