Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)limesema kuwa litaichukulia hatua za kinidhamu Yanga iwapo itabainika kuwa ilivunja kanuni za Ligi Kuu katika michezo yake miwili iliyopita dhidi ya Simba na Stand United.
TFF imeeleza hayo kutokana na kitendo cha mabingwa
hao wa kihistoria wa taji la Ligi Kuu, kutoingia kwenye vyumba vya
kubadilishia nguo katika mechi hizo mbili zilizochezwa Dar es Salaam na
Shinyanga katika kile kinachohusishwa na imani za kishirikina.
Ofisa wa Bodi ya Ligi wa TFF, Joel Balisidya
alisema kuwa kikao cha kamati ya nidhamu cha TFF kitakaa katika tarehe
ambayo itatangazwa hapo baadaye ili kupitia ripoti ya mechi hizo mbili,
kabla ya kuangalia adhabu gani ambayo Yanga watapewa iwapo walikiuka
kanuni zinazoendesha ligi.
“Kanuni za ligi ziko wazi kuwa iwapo timu imegoma
bila sababu maalumu kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, adhabu
gani inatakiwa itolewe. Hivyo, kama shirikisho tutakutana na kupitia
vifungu vinasemaje na tutatoa adhabu kama tukibaini uvunjifu wa kanuni
hizo,” alisema ofisa huyo.
Hata hivyo, alipotakiwa ataje tarehe ambayo kikao
hicho kitakaa, Balisidya alisema yeye hana mamlaka ya kupanga lini
kamati hiyo itakaa hivyo wafuatwe wahusika halisi.
Katika pambano dhidi ya Simba na lile la Stand United , Yanga iligomea kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.MWANANCHI
Post a Comment