0



OFISI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imemaliza kazi ya ukaguzi maalumu katika matumizi ya mabilioni ya shilingi katika Mamlaka ya Bandari (TPA). Akizungumza Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe alisema CAG amemaliza kazi yake na kukabidhi ripoti.

“Taarifa yenu ya mwaka jana ilikuwa na utata, ilionesha kulikuwa na matumizi ya fedha ya Sh bilioni 9.6 kwa ajili ya mkutano, Sh bilioni 9.4 kwa ajili ya matangazo na Sh bilioni 10 kwa ajili ya safari.

“Taarifa ya CAG tumeipata jana (juzi) hatujaisoma… natoa muda ili Kamati ipitie na pia na nyie muipitie vizuri,” alisema Filikunjombe.

Akitetea hoja ya kuomba CAG akague hesabu hizo hivi karibuni, Filikunjombe alisema Kamati ya PAC ilipotembelea TPA, ilikuta kwa mwaka mmoja mamlaka hiyo imetumia Sh bilioni tisa kwa ajili ya mkutano mkuu wa wafanyakazi.

“Tukawauliza hawa wajumbe wa mkutano mkuu wa wafanyakazi, kwanza mlifanyia wapi? Hapa hapa ndani (ya nchi)? Wako wangapi? Wako 180. Mmelipanaje mpaka inafika Sh bilioni tisa?” Alihoji.

Mbali na fedha hizo za mkutano wa wafanyakazi, Filikunjombe alisema pia walikutwa wametumia Sh bilioni tisa kwa matangazo.

“Tukauliza, haya matangazo mmetangaza wapi? Nje au ndani? Kwa sababu kama ni nje, labda. Kama ni ndani ya Tanzania matangazo ya Sh bilioni tisa, kila mmoja leo hii hata mtu ambaye yupo tumboni angeijua TPA,” alisema.

Kutokana na hali hiyo na kutokuwepo kwa muda wa kujadili taarifa hiyo ya CAG, Filikunjombe aliagiza Menejimenti ya Mamlaka ya Bandari (TPA) kwenda Dodoma kujadili ripoti hiyo na kutoa utetezi wao.

Wakati huo huo, Kamati hiyo imeitaka Bodi ya Chuo Kikuu cha Mzumbe, kufanyike uchunguzi katika ujenzi wa jengo la chuo hicho lililogharimu Sh bilioni 1.8, kama lilifuata taratibu za manunuzi.

Filikunjombe alisema wamefurahishwa na taarifa ya hesabu za chuo hicho, kwa sababu ni nzuri na mapato yao yalionesha kukua na kuongeza.

Kwa mwaka 2011-2012 mapato ya chuo hicho ya ndani yalionesha kufikia Sh milioni 600 ambapo kwa mwaka 2012-2013, yalipanda na kufikia Sh milioni 800.

Hata hivyo mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho, Daniel Mkude alisema kuwa Mzumbe inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa walimu, hali iliyowalazimu wakati mwingine kuajiri walimu wasio na viwango na kuingia gharama ya kuwasomesha.HABARILEO

Post a Comment

 
Top