0

UKUAJI wa uchumi na mabadiliko ya maisha ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara unaotokana na ugunduzi wa gesi asilia, unaanza kuwa dhahiri baada ya Kampuni ya Dangote Industries Limited, kuomba kibali cha kufua umeme wake wa megawati (MW) 75.

Umeme huo, unatarajiwa kutumika kwa ajili ya uzalishaji wa saruji katika kiwanda kinachojengwa mkoani humo na matumizi ya makazi. Jana Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Umeme (Ewura), ilitangaza ombi la kampuni hiyo kutaka leseni ya kufua umeme huo, ili umma ufahamu na kama kuna anayepinga, apeleke utetezi wake kabla ya kampuni hiyo kupewa leseni hiyo.

“Taarifa inatolewa kwa umma kwamba Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imepokea maombi ya leseni ya kuzalisha umeme kutoka Kampuni ya Dangote Industries Limited-Tanzania.

“Mtu yeyote mwenye maoni au pingamizi kuhusu maombi tajwa …afanye hivyo kwa maandishi na kuwasilisha Ewura kabla ya saa 11 jioni ya tarehe 14 ya Novemba 2014. Maombi hayo pamoja na maoni yanaweza kuoneshwa kwa mtu kwa maombi maalumu kwa maandishi siku sita kabla ya Novemba 21, 2014,” ilieleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, mitambo ya kufua umeme huo wa makaa ya mawe, itawekwa katika eneo la Pemba Mvita Mbuo, Kijiji cha Msijute wilayani Mtwara na utatumika kwa ajili ya uzalishaji wa saruji na makazi.

Umeme huo wa Kiwanda cha Dangote Industries Limited-Tanzania, ni mwingi kuliko mahitaji ya mikoa zaidi ya saba, ukiwemo mkoa wa Mtwara ambao peke yake unatumia megawati nane. Kwa sasa kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umeme (Tanesco), mkoa wa Manyara unatumia Mw 10, Singida (7), Lindi (5.5), Kigoma (6), Ruvuma (4.7) na Rukwa (6.8).

Hatua hiyo ya kiwanda hicho kinachomilikiwa na mfanyabiashara wa Nigeria, anayeongoza kwa utajiri barani Afrika, Aliko Dangote, inafanana na hatua aliyoichukua katika kiwanda kikubwa cha saruji duniani cha Dangote Cement Obajana Plant. Kiwanda hicho kilichoko katika eneo la Obajana, Jimbo la Kogi, kilometa 400 Kaskazini Mashariki mwa mji maarufu wa kibiashara wa Lagos nchini Nigeria, pia kinatumia umeme wake na kusaidia wakazi wanaokizunguka.

Mei mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete alipotembelea kiwanda hicho cha Obajana baada ya kushiriki Kongamano ya Uchumi Duniani-Afrika (WEFA), alimuuliza Dangote kama kiwanda hicho kinategemea kwa namna yoyote umeme wa Gridi ya Taifa.

Katika jibu lake mwekezaji huyo wa Nigeria alisema hawajaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, badala yake wamewekeza katika umeme wao unaowahakikishia umeme wakati wote na kwa kiwango ambacho wanakihitaji.

Mbali na kujenga miundombinu ya umeme wake, Dangote alisema kiwanda hicho pia kimejenga bwawa lake lenyewe kwa ajili ya huduma ya maji kusaidia uzalishaji wa saruji, bila kutegemea huduma ya maji ya Serikali. Bwawa hilo, ndilo linalotoa huduma ya maji kwa jamii inayozunguka kiwanda hicho.

Dangote pia alimuelezea Rais Kikwete kwamba kampuni yake inashiriki kwa karibu shughuli za jamii zinazozunguka kiwanda hicho. Miongoni mwa shughuli hizo kwa mujibu wa Dangote, ni pamoja na kutoa huduma za elimu kwa watoto na vijana wa wananchi wanaozunguka eneo hilo.

Katika kuboresha huduma hizo za elimu, Kampuni ya Saruji ya Dangote imejenga taasisi kubwa ya elimu ya Dangote Academy, ambayo itatoa elimu na mafunzo ya ufundi kwa ajili ya kuandaa wafanyakazi wa kiwanda hicho cha Nigeria na watoto wa jamii inayozunguka kiwanda hicho.

Pia wananchi hao na familia zao, wananufaika na huduma za maji na umeme, na tangu kiwanda kianzishwe mabenki 13 yalianzisha matawi yake katika eneo la kiwanda.

“Mheshimiwa Rais, mbali na nyumba za wafanyakazi, tunawajengea hata nyumba za kuishi wananchi wanaozunguka eneo hili ambao wanatuunga mkono sana,” alisema Dangote.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari alipofika Dar es Salaam hivi karibuni, mfanyabiashara huyo alisema watatafuta njia ya kukabili gharama zinazochangia bei ya saruji kuwa juu. Kwa sasa nchini, bei ya saruji hutegemea maeneo huku usafiri ukitajwa kuwa chanzo cha ongezeko hususani kwa mikoa ya pembezoni.

Wakati jijini Dar es Salaam, bei yake ni kati ya Sh 13,000 na 15,000 kwa mfuko wa kilo 50, baadhi ya mikoa, bei inazidi Sh 20,000. Pamoja na madai ya usafiri kuchangia gharama za saruji, bei hiyo ya juu pia imechangiwa na uwezo mdogo wa viwanda vinne vya ndani, ambavyo vimeshindwa kukidhi mahitaji.

Kwa sasa mahitaji ya saruji nchini ni tani milioni tatu kwa mwaka, wakati viwanda vilivyopo vina uwezo wa kuzalisha tani milioni 1.2. Kiwanda cha Dangote katika hilo, kimepanga kuzalisha tani milioni 3 na kuuza katika soko la ndani na nje.

Dangote pia alisema theluthi mbili ya wafanyakazi, watakuwa ni Watanzania na pia kutakuwapo na wafanyakazi wageni ambao hata hivyo hawatakaa milele, badala yake watakuwa na kazi ya kusaidia ujuzi na kiwanda kitakapotengamaa wataondoka.

Kiwanda hicho kikishaanza uzalishaji, kinatarajiwa kuwa na wafanyakazi 1,000 wa kudumu ambao watajengewa nyumba eneo la mradi, lakini pia kutakuwapo wafanyakazi wengine wapatao 9,000 wa kuja na kutoka.

Mbali na kiwanda hicho cha Dangote, taarifa za Serikali zinaonesha kampuni zingine 51 zimewasilisha maombi ya kuwekeza mkoani humo katika Kituo cha Uwekezaji (TIC).

Kampuni hizo na idadi ya miradi kwenye mabano ni mitambo ya luninga na redio (3), kilimo (2), usindikaji korosho (7), majengo ya kampuni na ofisi (2), majisafi (2) na bidhaa zitokanazo na saruji (3). Nyingine ni za mbolea (1), mikate (1), matangi ya mafuta (2), kiwanda cha ujenzi wa mabati (1), mbao (1), utalii (14), uchimbaji na watafutaji wa mafuta (1), usafirishaji (8) na plastiki (1).HABARILEO

Post a Comment

 
Top