0

Nachingwea. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, wamempa siku 14 mhandisi wa maji wa halmashauri hiyo, Bathromeo Matwiga awe amekamilisha mradi wa uchimbaji wa visima virefu vya maji wa Kijiji cha Naipanga.

Hatua hiyo imechukuliwa na madiwani hao baada ya mradi huo kutokamilika kwa zaidi ya miaka mitatu bila sababu za msingi kutolewa.

Kutokana na kushindwa kukamilika kwa mradi huo, kumewafanya wananchi kutembea mwendo mrefu kutafuta maji.

Wakizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani la halmashauri hiyo kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Diwani wa Kata ya Naipanga, Rashidi Chitawala alihoji sababu za mradi huo wa Sh40 milioni kukwama hadi sasa.

Kwa upande wake, Diwani Viti Maalumu, Veronica Makota alitaka kujua kama fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo kama kweli bado zipo, kama zipo kwa nini mradi umeshindikana hadi sasa.

Akitoa ufafanuzi wa malalamiko hayo, mhandisi Matwiga alikiri mradi huo kutokamilika kwa wakati kutokana na kusitishwa kufanya kazi mkandarasi aliyepewa kazi hiyo awali.

“Kwa sasa tumeanza mchakato wa kumtafuta mkandarasi mwingine kuendelea na mradi,” alisema Matwinga.

Na Christopher Lilai, Mwananchi

Post a Comment

 
Top