Na Owen Mwandumbya, Victoria Falls, Zimbabwe
Mkutano wa 36 wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi wanachama wa SADC
(SADC PF) ulioanza wiki hii mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe na
unatarajiwa kumalizika tarehe 3 Novemba, 2014, ikiwa ni baada ya
kukamilika kwa ajenda ya Mkutano huu pamoja na kufanyika kwa uchaguzi wa
Rais wa chama hicho atakayeongoza jukwaa hilo kwa miaka miwili ijayo.
Kauli mbiu ya mkutano huu ni “Bunge la kikanda la SADC – Wakati ni huu” ama kwa lugha ya kimombo inasema “ SADC Regional Parliament – the Future is Now”.
Maneno yaliyo katika kauli mbiu ya Mkutano huu yamebeba ujumbe
mzito sana wa Mabunge ya Nchi za SADC ikiwa ni dhamira ya dhati
waliyokuwa nayo wanachama hawa ya kuundwa kwa Bunge la kikanda
litakalokuwa na nguvu si tu ya kuzisimamia Serikali za Nchi Wanachama bali
pia kuwa na uhalali wa kuhakikisha kuwa maamuzi na hata mikataba
mbalimbali itakayofikiwa na chombo hiki katika ukanda huu vinatekelezwa
katika nchi wanachama.
Pamoja na kwamba yapo mengi yaliyojadiliwa katika Mkutano huu wa
Umoja wa Mabunge ya SADC hapa Zimbabwe, muhimu limekuwa ni uchaguzi wa
Rais wa Jukwaa hili ambaye ataongoza jitihada za kufanikisha malengo ya
chama hiki ya kufikia kuwa Bunge kamili ndani ya Miaka miwili ijayo
yanafanikiwa.
Spika wa Bunge la Tanzania
Mhe. Anne Makinda amekuwa akipigiwa chapuo na Wajumbe wengi wa Mkutano
ili aweze kukamata usukani wa kukiongoza chama hiki kwa miaka miwili
ijayo baada ya Rais wa sasa ambaye pia ni Spika wa Mauritius Mhe. Abdool
Razack Mahomed Ameen Peeroo, kumaliza muda wake. Kutokana na uungwaji
mkono mkubwa alionao Mhe. Makinda ameibuka kuwa mgombea pekee na hivyo
ni dhahiri atapitishwa na kukabidhiwa jukumu la kuongoza Jukwaa hili.
Msukumo wa Wajumbe wa Mkutano huu wa 36 kutaka Spika Makinda
aweze kuongoza Bunge hili unatokana na heshima na ushawishi mkubwa
ilivyonayo nchi ya Tanzania katika nchi wanachama wa SADC swala ambalo
linafanya wajumbe wengi wa Umoja huu waamini kuwa Mtanzania Makinda
atasaidia sana kusukuma masuala ya Jukwaa hili kwa Wakuu wa nchi
wanachama, kazi ambayo inahitaji mtu kutoka nchi inayokubalika na yenye
sifa za kidemokrasia ya kweli kwa na hivyo kuweza kupenyeza na
kufanikisha matakwa ya Bunge hili.
Kukubalika kwa Tanzania katika Ukanda wa huu wa Afrika Kusini na chapuo anayopigiwa Makinda ya kuongoza Bunge la SADC vinatokana na historia iliyoandikwa na Tanzania kupitia harakati za Ukombozi
wa Bara la Afrika kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1960. Kuanzia wakati
huo nchi ya Tanzania chini ya Uongozi wa hayati Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere, iliongoza mapambano ya ukombozi Barani Afrika
na kutoa msaada mkubwa kwa Vyama vya ukombozi vya nchi za Kusini mwa Afrika kama vile, Zimbabwe (ZANU), Afrika Kusini (ANC na PAC), Namibia (SWAPO), Angola (MPLA) na Msumbiji (Frelimo).
Post a Comment