Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe
Mheshimiwa Spika,
Siku ya Jana Vyombo vya Habari mbalimbali
vya Ndani na Nje ya Nchi vilitoa habari kwamba ujumbe wa Rais wa China
uliokuja nchini Miezi 18 iliyopita ulijihusisha na ununuzi wa pembe za
ndovu nchini. Chanzo cha habari hizo ni taarifa ya taasisi isiyo ya
kiserikali ya nchini Marekani ijulikanayo kama Environmental
Investigation Agency (EIA). Habari hiyo imekwenda mbali zaidi kuituhumu
nchi yetu na viongozi wake kutojali, wala kushughulikia tatizo la
biashara haramu ya pembe za ndovu.
Mheshimiwa Spika,
Ninapenda kupitia Bunge lako tukufu
kuutaarifu umma wa watanzania na dunia kwa ujumla kwamba madai
yaliyotolewa na NGO hiyo ya Marekani ya kuihusisha ziara ya kihistoria
ya Rais wa China kutembelea Tanzania kama nchi ya kwanza toka aingie
madarakani na biashara ya pembe za ndovu hayana ukweli wowote. Vilevile,
madai ya kwamba Serikali ya Tanzania haijali na wala haichukui hatua
dhidi ya wanaojishughulisha na biashara haramu ya pembe za ndovu sio
kweli.
Taarifa za EIA ni za kupikwa na
kuungwa kuungwa ili kuchafua heshima ya nchi yetu, pamoja na kuchafua
heshima ya rafiki zetu Taifa la China. Ni taarifa iliyoandaliwa na
kutolewa wakati huu ili kukidhi ajenda mahususi ambayo tunaifahamu fika.
Mheshimiwa Spika,
Kabla sijaelezea kwanini ninasema
taarifa hii sio ya kweli ningependa kwanza kulielezea Bunge lako tukufu
mambo sita yafuatayo ambayo hayana ubishi:
1) Moja, ni kweli soko kubwa la pembe za ndovu lipo China. Wanaofanya biashara haramu ya pembe za ndovu hutafuta soko China;
2) Ni ukweli usiopingika kwamba pembe
za ndovu nyingi zinazouzwa kwenye masoko haramu zinatokea Afrika,
Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi zinapotoka pembe hizo;
3) Biashara hiyo haramu inahusisha
wahalifu/ na mitandao ya waalifu ambao wana uraia wa nchi mbalimbali
zikiwemo China na Tanzania;
4) Serikali ya Tanzania na Serikali ya China hazifanyi biashara haramu ya pembe za ndovu na wala hazihusiki na mitandao haramu.
5) Kwa kutambua ukubwa wa Tatizo la
biashara hiyo haramu, Serikali zetu mbili zimekuwa na ushirikiano wa
karibu kabisa katika kukabiliana na mitandao inayofanya biashara hiyo
haramu. Vyombo vya dola vya nchi zetu mbili vimeshirikiana kwa karibu na
kupashana habari kila wakati zilizowezesha kuwakamata wahusika wa
biashara hiyo. Isitoshe wakati wa ziara iliyomalizika hivi majuzi
Serikali zetu mbili zilisaini mkataba wa kutupatia vifaa vya kusaidia
operesheni ya kupambana na ujangili wa wanyamapori – (China Aided
Equipment for Forest Resources and Wildlife Conservation). Vilevile
kwenye ziara hiyo tulisaini Mkataba wa kutupatia mitambo ya kisasa ya
kufanya ukaguzi wa mizigo bandarini- ambayo itasaidia kubaini mizigo
inayosafirishwa.
6) Tanzania na China zilishiriki
kikamilifu kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Kudhibiti Biashara Haramu ya
Pembe za ndovu (London Confrrence on Illegal Wildlife Trade) uliofanyika
mwezi Februari 2014. Moja ya mafanikio makubwa ya mkutano huo ni kwa
nchi za China, Botswana na Tanzania kusaini mkataba wa kupambana na
biashara hiyo haramu. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa China kusaini
Mkataba wa aina hiyo, jambo linalodhihirisha umakini wa Serikali ya Rais
Xi Jinping kushughulikia tatizo la biashara haramu. Vilevile kabla ya
mkutano huo wa London, Serikali ya China ilichoma moto hadharani shehena
ya meno ya tembo haramu yaliyokuwa yakishikiliwa nchini humo.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya kusema hayo, naomba sasa nitoe sababu kwanini ninasema habari za NGO ya EIA ni za uongo;
Mheshimiwa Spika,
Taarifa kama hii iliyotoka kwenye New
York times sio mara ya kwanza kutolewa. Taarifa ya aina hii iliwahi
kutolewa mwaka jana. Mtoa taarifa ambaye ametajwa kuwa chanzo cha habari
ni mtu mmoja ambaye walimkuta barabarani na kuanza kumuuliza maswali.
Mtu huyo sio mtumishi wa bandari wala uwanja wa ndege. Ni mpita njia tu
wa mtaani. Hata video ya mahojiano inaonyesha hivyo. Ukiachilia mbali
uwongo uliotolewa na bwana huyo, taasisi ya EIA imeongelea tukio la
kontena lililokamatwa Bandarini likiwa na pembe za ndovu.
Ni kweli kabisa kwamba kontena la
pembe lilikamatwa bandarini na vyombo vya dola. Jambo moja ambalo watu
wengi hawalijui ni kwamba mafanikio ya operesheni ile yalitokana na
ushirikiano wa vyombo vya usalama vya Tanzania na China. Taarifa za
kiinteligensia juu ya operation hiyo zilitoka China na kuwasilishwa
Tanzania ndio operesheni ikafanikiwa. Lakini habari zilizotoka kwenye
mitandao zilisema kwamba Kontena limekamatwa likipelekwa kwenye meli ya
kijeshi ya China...jambo ambalo sio kweli.
Mbali na hayo, ziara ha Rais Xi
nchini ilikuwa ya masaa 24, na programu yake ilianza mara tu alipowasili
nchini kuanzia saa 9 alasiri hadi saa 4 usiku kwenye dhifa ya taifa.
Siku ya pili ratiba ilianza asubuhi kwa uzunduzi wa Ukumbi wa Mikutano
ya Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere. Baada ya hapo Rais Xi na Ujumbe
wake walikuwa na mikutano na Rais wa Zanzibar Mhe Dk.Ali Mohamed Shein
na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mhe Benjamin William Mkapa. Baada ya
hapo Rais Xi na ujumbe wake walienda kwenye makaburi ya Wachina kule
Majohe na kisha wakaondoka kwenda uwanja wa ndege. Sasa hizo shopping
zinazoelezewa kufanywa na ujumbe wa rais Xi zilifanyika saa ngapi?
Jambommuhimu kujiuliza, je hiyo
taarifa ya Rais Xi na ujumbe wake kubeba pembe za ndovu iweje itoke leo?
Kwanini wakati huu baada ya ziara ya Rais wetu nchini China? Kwanini
itoke baada ya Mhe Rais kuhutubia mafanikio ya ziara yake nchini China?
Mheshimiwa Spika,
Jibu kila mmoja anaweza kujua.
Wasambazaji wa taarifa hizi hawaitakii mema nchi yetu. Hawawatakii mema
marafiki zetu wa China. Wamejawa na wivu na husuda kwa mafanikio ya
China. Inashangaza kuona, wanawachukia huku wanawategemea. Wao
wangependa wao peke yao wafanye biashara na China, wakachukue mikopo
China, wavutie uwekezaji kutoka China, lakini tukifanya sisi waafrika
inakuwa nongwa. Tusikubali upuuzi wa aina hii. Sisi ni taifa huru,
hatutachaguliwa marafiki wala hatutarisishwa maadui. Tutaendeleza
ushirikiano wetu wa kidugu na China na wala hatutorudi nyuma kamwe
kutoka na maneno ya uwongo na uzushi.
Aidha, ninapenda kulihakikishia Bunge
lako Tukufu Mheshimiwa Spika kwamba Serikali yetu haitorudi nyuma.
Tutaendeleza mapambano dhidi ya biashara haramu ya pembe za ndovu. Wale
wote wanaoshughulika na biashara hizo, siku zao zimefikia mwisho.
Ahsanteni kwa kunisikiliza
Post a Comment