0
“NINAPENDA niwahakikishie ninyi wanahabari na umma wa Watanzania kuwa kazi hii itafanyika kwa uangalifu mkubwa na inatarajiwa kukamilika kwa muda uliopangwa”.
Hiyo ni kauli  ya   Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliyotolewa hivi karibuni wakati wa   mkutano wake na  waandishi wa habari, ambapo ilitoa taarifa kwamba ilikwishaanza  na inaendelea na mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
NEC inafafanua kuwa majaribio ya uboreshaji wa daftari hilo yataanza rasmi katikati ya ya Novemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa NEC, majaribio hayo yatafanyika kwa kutumia mfumo mpya wa ‘Biometric Voter Registration’ (BVR) katika majimbo matatu ya uchaguzi ya Kawe katika Manispaa ya Kinondoni, Kilombero na Mlele ambapo vituo vya uandikishaji vimewekwa katika kata zilizomo katika majimbo husika.
Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji mkuu mstaafu wa Zanzibar, Hamid   Mahamoud Hamid anasema kuwa; “Tume tayari imekwisha pokea baadhi ya vifaa muhimu vya uandikishaji zikiwemo fomu za uandikishaji, hivyo kinachosubiriwa ni kupokea BVR kits 250 zinazotarajiwa kupokelewa wakati wowote.
“Uandikishaji utakapoanza, vituo vitafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni, vyama vya siasa vinaruhusiwa kuweka mawakala wao katika kituo ili kushuhudia jinsi uandikishaji utakavyokuwa unafanyika,”alisema.
Kwamba baada ya majaribio hayo kukamilika, kazi rasmi ya uandikishaji itaanza katika maeneo yote nchini.
“Tunatarajia uboreshajiwa wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika kwa wakati mmoja katika mikoa yote nchini, isipokuwa Dares Salaam na Zanzibar. Uandikishaji katika mikoa maeneo haya utafanyika baada ya kukamilika katika mikoa mingine. Muda wa uandikishaji utakuwa ni siku saba katika kila kituo,” alisema.
Aliongeza kwamba uandikishaji katika mikoa yote umepangwa kufanyika kuanzia mwanzoni mwa Januari mwaka hadi katikati ya Februari mwaka huu, wakati katika mikoa ya Dar es Salaam na Zanzibar utafanyika mwishoni mwa Februari na kukamilika Machi mwaka huu.
Kwa mujibu wa makamu huyo, uandikishaji huo utafanyika katika awamu nne kwenye kila halmashauri ili kutoa fursa ya kuhamisha vifaa vya uandikishaji kutoka eneo moja kwenda eneo lingine.
“Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utahusisha wapigakura wote, wapya na wazamani. Wapigakura wa zamani yaani wale ambao walikuwa wamejiandikisha  katika daftari la zamani, watatakiwa kwenda katika vituo vya kujiandikisha vilivyoko karibu na maeneo wanayoishi ili kuchukuliwa taarifa zao hasa alama za vidole, picha na saini zao kuingizwa katika mfumo Biometric Voter Registration na hatimaye watapewa vitambulisho vipya,” alisisitiza.
Anasema wapigakura ambao watakuwa na kadi zao za kupigakura za zamani watatakiwa kwenda na kadi zao katika kituo cha kujiandikisha ili kurahisisha kuhamisha taarifa zao za awali katika mfumo mpya wa BVR.
Kwa mujibu wa NEC, wapigakura waliopoteza kadi au wale ambao kadi zao zimeharibika watatakiwa kwenda kituoni ili kujiandikisha na kupewa kadi mpya.
Jaji Hamid anafafanua kuwa wapigakura wenye vitambulisho vya taifa jijini Dar es Salaam na Zanzibar watakuja na kadi zao ambazo taarifa zao zitasomwa na vifaa maalum ili kupunguza muda utakaotumika katika kazi hiyo, pia watapewa kadi mpya ya mpigakura.
Kwa wapigakura wanaoishi na ulemavu na wale ambao hawajui kusoma na kuandika wanaruhusiwa kwenda kituoni na mtu mmoja katika familia wanayemuamini ili kusaidia katika uandikishaji.
“Uboreshaji huu unahusisha pia kuandikisha wapigakura wote waliotimiza umri wa miaka 18 au zaidi na wale ambao ifikapo siku ya upigaji kura ya maoni na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, watakuwa wametimiza umri wa miaka 18. Pia wale wote ambao kwa sababu mbalimbali hawakuwahi kujiandikisha katika daftari wataandikishwa,” anasisitiza.
Kwamba jumla ya watu wenye umri wa miaka 18 na zaidi wapatao milioni 23.09 wanatarajiwa kujiandikisha katika daftari hilo.
Julius Malaba ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, ambaye anasema tayari kiasi cha sh. bilioni 15 kimetolewa na seriklai kwa ajili ya kazi hiyo, na kwamba mradi mzima utagharimu zaidi ya sh. bilioni 270.TANZANIADAIMA

Post a Comment

 
Top