Dar es
Salaam. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), jana iligeuka
‘mwiba mkali’ kwa watendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC), Kampuni ya Ranchi ya Taifa (Narco) na Wizara ya Nishati na
Madini, baada ya kuwatimua wakurugenzi na wenyeviti wa bodi kwa
kushindwa kutoa maelezo ya kina kuhusu ubadhirifu wa fedha za umma,
uzembe na wizi.
Katika
uamuzi wake, kamati hiyo chini ya mwenyekiti wake, Zitto Kabwe
iliwatimua watendaji wa TPDC baada ya kushindwa kuwasilisha mikataba 26
ya gesi na mapitio yake kama walivyoagizwa na kamati hiyo mwaka mmoja
uliopita.
Huku
‘wakijikanyaga’ kujibu maswali, Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Michael
Manda na Kaimu Mkurugenzi wa shirika hilo, James Andilile wametakiwa
kuwasilisha mikataba hiyo katika kamati ya PAC kesho, baada ya saa za
kazi ili kupangiwa siku ya kukutana na kamati hiyo.
Zitto
alianza kwa kumtaka Manda na Andilile kueleza sababu za kutowasilisha
mikataba hiyo na kujibiwa kwamba mikataba ya Serikali ina utaratibu wake
wa kuipata, huku wakisema kwa Kamati ni kupitia ofisi za Bunge.
Walisema kuwa aliyetoa agizo la kutakiwa kwa mikataba hiyo ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Kauli hiyo
ilichafua hali ya hewa katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika
katika ofisi ndogo za Bunge jijini hapa na kumlazimu Zitto na Makamu
wake, Deo Filikunjombe kueleza kuwa Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya
Bunge inaruhusu kamati kupata taarifa yoyote ile.
“Taarifa
ambazo zinaweza zisifike katika kamati ni zile zinazohusu mambo nyeti ya
usalama wa nchi. Hata hivyo, taarifa hizo zinaweza kufika katika
kamati, lakini akaonyeshwa mwenyekiti tu. Mnajua tunaweza kuwapa adhabu
kali kwa kuinyima kamati nyaraka na kuizuia kufanya kazi,” alisema
Zitto.
Licha ya
onyo hilo, Manda na Andilile kwa nyakati tofauti walijitetea kuwa
nyaraka hizo za mikataba ya gesi zipo, lakini hawakwenda nazo katika
kamati hiyo, huku wakirejea kauli yao kwamba kiutaratibu zinatakiwa
kupitia ofisi za Bunge.
“Tunataka
kujua huo utaratibu mmeutoa wapi kwamba nyaraka zikitakiwa na kamati
lazima zipitie katika ofisi ya Bunge. Mwaka umepita na hamjaleta nyaraka
hizo. Sasa kama nyaraka anazo Profesa Muhongo mbona hamjaja naye hapa
hata na Katibu wake (Maswi) Eliakim,” alihoji Filikunjombe.
Akijitetea, Manda aliomba kamati kutowachukulia adhabu kali na kuahidi kuziwasilisha nyaraka hizo kama walivyoagizwa.
Katika hatua
nyingine, PAC ilieleza ubadhirifu wa maeneo matatu unaodaiwa kufanyika
Narco na kusababisha kupotea zaidi ya ng’ombe 360 ndani ya miezi mitatu
na kukwama kwa ujenzi wa machinjio ya kisasa.
Wakati
ubadhirifu huo ukielezwa, Narco iliwasilisha ombi katika kamati hiyo
ikiomba Sh17 bilioni serikalini kwa ajili ya kuongeza mtaji wake.
Akitoa
maagizo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Narco, Salum Shamte, Filikunjombe
alisema kamati yake haijaridhishwa na maelezo ya kampuni hiyo na kuipa
wiki tatu iwe imetoa majibu ya maeneo hayo matatu, ili kujua hatua
zinazoweza kuchukuliwa.
“Sisi kama
kamati hatuwezi kuiagiza Serikali iwape fedha nyingine. Kwanza
hamkopesheki, kwa hali halisi, mkipewa Sh17 bilioni mnazozitaka nazo
zitapotea kama hizo nyingine. Tunakwenda kusema bungeni kwamba msipewe
hata shilingi mpaka mtakapobadilika,” alisema Filikunjombe.
Alisema watawasiliana na msajili wa Hazina kujua hatua za kuchukua kwa sababu wamebaini kuwa shida ya Narco ni menejimenti.
“Pia umri wa
kustaafu ni miaka 60, lakini hapa tunaona Mkurugenzi Mtendaji wa Narco
(Dk John Mbogoma) ana miaka 61. Mtueleze kwa nini anaendelea kuwepo
kazini wakati umri wake wa kustaafu ulishapita,” alisema.
Pia alisema
katika kipindi hicho cha wiki tatu watawasiliana na msajili wa Hazina,
ili kujua kama mwenyekiti wa bodi (Shamte), anastahili kuendelea kushika
nafasi hiyo.
Wizara ya Nishati
Kutokana na
Wizara ya Nishati na Madini kutokuwa na maelezo ya kuridhisha kuhusu
fedha za kulipa matangazo ya bajeti ya wizara hiyo katika vyombo vya
habari, Zitto aliagiza Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), kufanya ukaguzi wa malipo hayo.
Katika
maelezo yake, Maswi alifafanua Sh400.65 bilioni kati ya Sh648 bilioni ya
fedha za maendeleo zilivyotumika kugharimia mpango wa dharura wa umeme
pamoja na deni.
Pia alieleza utaratibu wa ulipaji wa madeni wa TPDC kwa kampuni za Songas na Pan Afrika.
Na Fidelis Butahe na Andrew Msechu, Mwananchi
Post a Comment