Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
----
Na Boniface Meena, Mwananchi
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema hatua ya viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuingia katika makubaliano ya kushirikiana “ni kaburi la vyama hivyo.”
Wakati
Nape akisema hayo, baadhi ya wasomi wamesema ni hatua kubwa lakini
yenye kuhitaji kuwa na sera na itikadi ya pamoja. Akizungumza kwa simu
jana, Nape alisema Ukawa ni kaburi la vyama vya upinzani vilivyoungana
kwa kuwa vitapoteza utambulisho wao.
“Huu ni mwanzo wa kumomonyoka kwa vyama vya upinzani, moja vyama hivyo vitapoteza identity (utambulisho) zao na kama mkutano wenyewe ndiyo umehudhuriwa na watu kidogo vile, basi hali yao ni ngumu sana,” alisema Nape.
Alisema
kutakuwa na mgogoro mkubwa hasa kwenye nafasi za kugombea kwa kuwa
hasa katika majimbo akitolea mfano wa Jimbo la Ubungo ambalo alisema Julius Mtatiro wa CUF anataka kugombea huku John Mnyika wa Chadema naye akitaka kutetea nafasi yake.
“Ukawa ni bomu ambalo litawalipukia na kwangu sijaona jambo jema kwa ushirikiano huo,” alisema Nape.
Hata hivyo, Nape alisema jambo moja ambalo vyama hivyo vimelifanya ni kuunganisha nguvu kupambana na CCM ambayo misuli yake ni mikubwa.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kitila Mkumbo alisema ushirikiano huo ni hatua kubwa kwa kuwa angalau umeweza kuainisha mambo ambayo watashirikiana.
Hata
hivyo, Profesa Mkumbo alisema hiyo iwe ni hatua ya kwanza kushirikiana
na hatua ya pili iwe ni kwa vyama vya upinzani kuungana kabisa na kuwa
chama kimoja kiitikadi na kifalsafa ili kuweza kuwa na vyama viwili
vikubwa nchini.
“Nilidhani
wangekuwa na sera ya kuweza kuchambua tofauti za kiitikadi ndani ya
vyama na kuja na vipaumbele vya msingi katika nchi, lakini ushirikiano
huo unaonekana ni wa kimadaraka zaidi,” alisema Profesa Mkumbo.
Alisema
itikadi za vyama ni muhimu kuzingatiwa kwa kuwa ni jambo la msingi
katika kuunda Serikali. “Ukiangalia Chadema wao itikadi yao ni ya
kibepari, CUF ni kiliberali na NCCR-Mageuzi ni ujamaa, sasa wakiunda
serikali itakuwa ya itikadi gani? Hili ni jambo la kujiuliza,” alisema.
Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM, Dk Benson Bana alisema si jambo baya lakini kinachohitajika ni kujulikana wamejenga ushirikiano huo kwa msingi gani.
“Hamuwezi
kuungana kwa sababu ya kwenda Ikulu. Tunahitaji wawe na itikadi ya
aina moja na sera za mbadala ingekuwa ni jambo jema zaidi,” alisema Dk
Bana na kuongeza: “Wakubaliane sera za mambo mbalimbali ambayo yataweza kuing’oa CCM na si kujiwekea mkakati wa kugawana madaraka.”
Post a Comment