0
Dar es Salaam. Kocha mkuu wa Tanzania Prisons, David Mwamaja amesema Simba ilikosa umakini baada ya kutaka kulinda bao, hivyo kucheza kwa kujihami kuliko kushambulia na kuwaruhusu wenyeji kusawazisha.


Akizungumza na gazeti hili jana, Mwamaja alisema alibaini mbinu ya Simba hivyo kulazimika kubadili mfumo wa 1-4-3-2 alioanza nao na kutumia mfumo wa 4,3,3 ambao uliwasaidia ‘kuikamata’ Simba kwenye mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.


“Simba ilipopata bao la kuongoza ilijihami hivyo nikatumia udhaifu huo kubadili fomesheni yangu na kuongeza watu wa kushambulia na kufanikiwa kusawazaisha,” alisema kocha huyo.


Alisema kwenye mpira hakuna mbinu mbaya kama kujihami na ndiyo iliwaponza Simba na kusisitiza kuwa kipindi cha pili wapinzani wao hawakuwasumbua kwa kuwa tayari alishabaini udhaifu wao na kuutumia.


Kocha wa Simba, Patrick Phiri alisema mechi hiyo imemvuruga kwani hakutarajia kutoka sare kwa mara nyingine na kusisitiza kuwa timu yake ilicheza kwa presha.


“Wachezaji wangu walicheza kwa presha, hawakuwa makini kabisa na mechi ile. Matokeo haya yamenivuruga sana, sikutarajia kupata sare ya tano mfululizo,” alisema Phiri ambaye kwenye mechi hiyo alitumia mfumo wa 4-4-2.


Kwa mujibu wa kocha huyo, kikosi hicho kitabaki Iringa ambako kitaweka kambi na Ijumaa kitatokea Iringa kwenda Morogoro tayari kwa mchezo wao wa Jumamosi.


Simba imetoka sare mara tano mfululizo na ina pointi tano, imefungwa mabao matano na kushinda matano kwenye mechi tano ilizocheza dhidi ya Polisi Morogoro, Coastal Union, Stand United, Yanga na Tanzania Prisons.MWANANCHI

Post a Comment

 
Top