0
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema mfumo mpya wa uandikishaji wa wapiga kura wa ‘Biometric Voter Registration Kit’ (BVR), utatumika kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura tu, si kwa ajili ya upigaji kura kielektroniki.
Hayo yalielezwa jana na Kamishna wa Tume hiyo, Mchanga Mjaka wakati akifungua Mkutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na waandishi wa habari wa jijini Mwanza juu ya uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura.
Alisema kwa kutumia mfumo huo mpya, wananchi wote wenye sifa za kuwa wapiga kura na wale wenye kadi za mpiga kura, watatakiwa kuandikishwa upya.
Alisema mfumo wa BVR ni wa kuchukua au kupima taarifa za mtu za kibaiolojia au tabia ya mwanadamu na kuzihifadhi katika kanzi data kwa ajili ya utambuzi, ambapo hutumika katika kumtambua mtu na kumtofautisha na mwingine.
“Mfumo huu utasaidia kuwa na daftari sahihi na linaloaminika zaidi kwa ajili ya upigaji wa kura za maoni na uchaguzi mkuu mwaka 2015,” alisema.
Alisema Tume ina mategemeo makubwa kuwa matumizi ya BVR, yatapunguza ama kuondoa matatizo yaliyomo kwenye daftari lililopo, ikiwa ni pamoja na kuzuia mtu kujiandikisha zaidi ya mara moja. Alisema vifaa kwa ajili ya zoezi hilo, vimekwishaagizwa na vitapokelewa mapema mwezi Agosti mwaka huu.
Akiwasilisha mada ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa kutumia teknolojia ya BVR, Mkuu wa Idara ya Uchaguzi, Clotilda Komba alisema uamuzi wa matumizi ya BVR umefikiwa kutokana na changamoto zilizojitokeza katika matumizi ya teknolojia ya awali ya Optical Mark Recognition (OMR) ambazo ni pamoja na kuwepo kwa majina ya watu waliofariki katika daftari.
Changamoto nyingine ni majina ya wapiga kura kutoonekana kwenye daftari siku ya kupiga kura wakati walijiandikisha na wana kadi zao za kupiga kura na kuwepo kwa majina ya watu waliojiandikisha zaidi ya mara moja.

Post a Comment

 
Top