BAADHI
ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, wamelalamikia bei kubwa za vyakula
katika kipindi hiki cha Mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwenye
badhi ya masoko jijini humo.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, wakazi wa jiji hilo Bw. Khamis Mshaka na Bi. Salma
Jumbe, walisema baadhi ya wafanyabiashara wanapandisha bei ya vyakula
ili kupata faida.
Walisema hali hiyo inawafanya wananchi wengi hasa wenye kipato kidogo washindwe kumudu bei za vyakula wanapokwenda sokoni.
“Tabia
hii si nzuri na imekuwa ikijitokeza mara kwa mara unapofika wakati wa
mfungo...bidhaa zilizopo sokoni si za Waislamu pekee, hivyo tunaziomba
mamlaka husika zichukue hatua,” walisema.
Bi.
Jumbe alisema, baadhi ya wafanya biashara wanaficha vyakula kwenye
maghala ili siku zinavyozidi kwenda, waviuze kwa bei kubwa jambo ambalo
serikali inapaswa kulifanyia uchunguzi ili kukomesha tabia hiyo.
Kwa
upande wake, Bi.Maria Albert ambaye ni mamalishe, anayefanya biashara
ya kuuza chakula kwenye Mtaa wa Kongo, Kariakoo, alisema kutokana na bei
kubwa ya vyakula, wanashindwa kupata faida.
Kutokana
na malalamiko hayo, Mpekuzi ilitembelea kwenye baadhi ya masoko kama
Kariakoo, Buguruni, Tandika, Ilala, Kisutu na kubaini baadhi ya
wafanyabiashara wanauza vyakula kwa bei kubwa. Bw. Ally Gumbo ambaye ni
mfanyabiashara wa mihogo, viazi na magimbi katika Soko la Kariakoo,
alisema bei ya mihogo na magimbi imepanda kutokana na kupandishiwa bei
na wakulima.
Alisema
bei ya sasa kwa mhogo mmoja ni kuanzia sh .1,000 kutokana na ukubwa
wake ambapo magimbi ni sh. 3,000 kwa sado moja tofauti na awali ambapo
ilikuwa ni sh.1, 500.
Naye
Bw. Brown Sanga, mfanyabiashara wa nafaka katika Soko la Kisutu,
alisema ni dhambi kupandisha bei za vyakula katika kipindi hiki cha
Mfungo wa Ramadhani.
“Wafanyabiashara
tunapaswa kuwa na ubinadamu hata kama tunatafuta pesa, tunatakiwa
kusaidiana ili ndugu zetu Waislamu tusiwaweke katika mazingira magumu ya
kutafuta futari,”alisema.
Post a Comment