0
jakaya_kikwete
Kwa mara ya pili ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, Rais Jakaya Kikwete juzi alionyesha kuchoshwa na vitendo vya ubadhirifu katika vyama vya ushirika na kuliagiza Jeshi la Polisi kuanza upelelezi wa viongozi wa vyama hivyo na maofisa ushirika wanaosababisha wakulima kunyimwa haki zao. Katika hatua ya kwanza, Jeshi la Polisi limeagizwa kuwakamata wezi wa fedha za wakulima wa tumbaku mkoani Tabora na kuwafikisha mahakamani haraka iwezekanavyo.

Rais alitoa agizo hilo mkoani Tabora katika hotuba yake ya uzinduzi wa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti. Katika hali iliyoonyesha kwamba uvumilivu wake kwa vitendo vya wizi wa fedha na mali za wakulima umefika kikomo, Rais Kikwete mara baada ya kutoa hotuba ya uzinduzi huo, alijielekeza katika kulaani vitendo hivyo na kusema haingekuwa vyema iwapo asingezungumzia wizi katika chama cha ushirika mkoani humo.


Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwake kuonyesha kuchoshwa na vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi ya viongozi na maofisa katika vyama vya ushirika nchini. Julai mwaka uliopita, Rais Kikwete alisema wakati akizindua jengo la kitega uchumi la Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Kagera (KCU), mjini Bukoba kwamba baadhi ya vyama vya ushirika vina mkusanyiko wa wezi wanaotafuna fedha za wananchi hata “bila kunawa mikono”. Katika hotuba yake mjini Tabora juzi, Rais alisema Serikali imechoshwa na wezi wa fedha za wakulima wa tumbaku na haitakuwa na huruma tena kwa wote watakaobainika.


Kauli hiyo ya Rais inaonyesha kwamba pengine Serikali yake imekata tamaa katika juhudi zake za kuvirekebisha vyama hivyo, baada ya muda mrefu wa ufisadi na ubadhirifu wa mali na fedha za wakulima. Ni kauli iliyojaa hasira na inayoonyesha kwamba Rais bila shaka amevunjika moyo kutokana na kukwama kwa juhudi zake za kuvirudisha vyama hivyo katika mstari nyoofu.


Ikumbukwe kwamba katika kuonyesha dhamira yake ya kuvifufua vyama hivyo, Rais Kikwete katika muhula wake wa kwanza wa uongozi aliamua kulipa madeni yote ya vyama vya ushirika, akitegemea hatua hiyo ingevikwamua kutoka katika madeni yaliyokuwa yamevielemea. Jambo linalomfadhaisha hivi sasa ni kuona vyama hivyo vikijitumbukiza tena katika madeni makubwa kutokana na viongozi wake kuendeleza ubadhirifu wa fedha na mali za vyama hivyo.


Ni bahati mbaya kwamba Serikali imechelewa na hivyo haina uwezo tena wa kuvirudisha katika mstari nyoofu. Karipio la Rais Kikwete mwaka jana kwa viongozi wa vyama hivyo iliishia tu mjini Bukoba, kwani haikufuatiwa na utekelezaji wowote. Hatuoni kama hatua ya Rais, ya kulitaka Jeshi la Polisi kwenda Tabora kuchunguza na kuwaburuza mahakamani watuhumiwa wa ubadhirifu huo, itamaliza tatizo hilo kwani tatizo la wizi katika vyama vya ushirika ni la nchi nzima, siyo Tabora pekee.


Upo ushahidi kwamba Serikali imelea wezi hao, kwani baadhi ya mawaziri na watendaji serikalini wamekuwa pia wakijihusisha na ubadhirifu huo. Vyama hivyo haviwajibiki tena kwa wakulima na vimeshindwa kuwatafutia masoko na bei nzuri za mazao yao. Kwa kuwa Rais amebakiza muda mfupi kumaliza ngwe yake ya uongozi, wakulima watalazimika kuvuta subira hadi baadaye mwaka ujao kuona mwelekeo na hatima ya vyama vyao vya ushirika.MWANANCHI

Post a Comment

 
Top