0
http://www.ibn-tv.com/wp-content/uploads/2013/07/Rais-Kikwete1.jpg
RAIS JAKAYA KIKWETE.

WIZI na ubadhirifu katika vyama vya ushirika, mwisho wake upo karibu baada ya Rais Jakaya Kikwete kuagiza Jeshi la Polisi, kuanza upelelezi wa maofisa ushirika wanaoshiriki vitendo hivyo na kuwanyima wakulima haki zao. Rais Kikwete alitoa agizo hilo juzi mkoani Tabora, wakati wa ufunguzi wa huduma za uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na ya matiti mkoani hapa.

Akizungumzia tatizo la wakulima wa tumbaku kutolipwa stahili zao na vyama vya ushirika, Rais Kikwete alisema ameelezwa na kulielewa vizuri tatizo hilo.

Vijana wa IGP “Kuna tuhuma za wizi na ubadhirifu. Nimemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi (Ernest Mangu), atume watu wake wa upelelezi wa makosa ya jinai, waje wafanye uchunguzi ili wahusika wakamatwe na kufikishwa mahakamani na kupewa adhabu zinazostahili.

“Ameniahidi kuwa kesho kutwa Jumatatu, watu hao watakuja. Wapeni ushirikiano unaostahili ili tukomeshe uhalifu na dhuluma zinazofanywa na maofisa wa vyama vya ushirika na taasisi za fedha kwa muda mrefu sasa,” alisema Rais Kikwete.

Hatua hiyo ya Rais Kikwete, imekuja baada ya baadhi ya wakulima wa tumbaku mkoani Tabora mwishoni mwa mwezi uliopita, kulalamika kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kuhusu vyama vya ushirika na wanunuzi wanavyodhulumu fedha zao kila msimu.

Baada ya kuelezwa namna dhuluma hiyo ilivyofanyika, Kinana alisema kilio cha wakulima hao, atakifikisha kwa Rais Kikwete, ili achukue hatua zaidi za kisheria.

Malalamiko Kinana ambaye yuko katika ziara ya siku 26 ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika mikoa ya Tabora, Singida na Manyara, alielezwa namna dhuluma hiyo inavyofanyika, alipokuwa katika Kijiji cha Mgambo, Kata ya Kitunda wilayani Sikonge mkoani Tabora.

Mkulima wa tumbaku, Juma Kaseka, alidai vyama vya ushirika pamoja na wanunuzi, wamekuwa wakishirikiana kudhulumu na kuibia wakulima mamilioni ya fedha kila msimu. Aidha alilalamikia Serikali kwa kushindwa kuwachukulia hatua vigogo wa vyama vya ushirika waliotuhumiwa kutafuna Sh bilioni 28 za wakulima.

Alidai pamoja na ripoti ya ukaguzi wa wizi wa mamilioni hayo ya wakulima kufika serikalini, hakuna hatua kama za kuwafukuza kazi na kuwafikisha mahakamani zilizochukuliwa.

Usafirishaji, maghala Mbali na hiyo, Kaseka alilalamikia gharama za usafirishaji wa pembejeo kutoka Dar es Salaam mpaka Tabora, ambapo alisema mfuko mmoja wa pembejeo unasafirishwa kwa Sh 12,000 tofauti na saruji ambao unasafirishwa kwa Sh 2,000.

Alidai kuwa mbinu hiyo ya usafirishaji wa pembejeo, inafanywa na maofisa wa vyama vya ushirika kutoka wizarani. Katika orodha ya malalamiko hayo, Kaseka pia alidai kuwa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia tumbaku uliogharimu mabilioni ya fedha, hauna kiwango na ulijengwa chini ya kiwango.

Kwa mujibu wa madai hayo ya Kaseka, maghala hayo yameanguka chini huku gharama za ujenzi wa maghala hayo zikitakiwa kulipwa na wakulima, jambo linalowazidisha umasikini.

Matumizi ya dola Kaseka aliendelea kufafanua namna dhuluma hiyo inavyofanyika na kuongeza kuwa, wakulima wanatakiwa kulipa kwa dola za Marekani katika kuchangia gharama za ujenzi, wakati wao wanalipwa kwa Shilingi ya Tanzania tena kwa mkopo.

Kwa upande wake, mkulima Nasibu Baraka, kutoka wilaya ya Uyui, alisema zao la tumbaku mkoani Tabora halijawaondolea umasikini wakulima na kwamba tatizo hilo linahitaji kupatiwa ufumbuzi na Serikali.

Alidai migogoro mingi inayowakabili wakulima wa tumbaku katika wilaya hiyo, inasababishwa na viongozi wa vyama vya ushirika na kuwa viongozi hao wamekuwa wakibebwa, wakati inafahamika kuwa wanatafuna mabilioni ya fedha na kuwabebesha madeni wakulima.

Mkulima Jayunga Magina, mkazi wa Kijiji cha Utuluma, alitaka waliohusika na ubadhirifu huo wa fedha, wachukuliwe hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

Kukopwa Alidai baadhi ya wakulima hawajalipwa kwa zaidi ya miaka miwili na kusababisha maisha yao yazidi kuwa magumu, huku vigogo waliotafuna fedha hizo wakiendelea kuishi maisha mazuri.

Suleimani Salehe mkazi wa Sikonge, alidai alianza kulima tumbaku mwaka 1969, lakini kila mwaka pembejeo za zao hilo zinapanda, huku mkulima Michael Vicent, akidai pembejeo za tumbaku wanapewa matajiri na wakulima wadogo wananyimwa.

Malalamiko ya RC Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatuma Mwasa alisema asilimia 80 ya wakazi wa Tabora ni wakulima na kwamba asilimia 65 ya tumbaku inayolimwa Tanzania inazalishwa mkoani humo.

Alisema msimu wa kilimo wa mwaka 2012-2013 mkoa ulipata mkopo wa Sh bilioni 112.6 kupitia benki za NMB na CRDB kutokana na benki hizo kupewa dhamana ya Serikali kwa ajili ya pembejeo za kilimo.

Kwa mujibu wa Fatuma, ununuzi mkubwa wa pembejeo za Sh bilioni 90, ulifanywa na kigogo mmoja wa vyama vya ushirika (hakumtaja jina) bila kupitishwa na mkutano mkuu wa vyama vya ushirika.

Alisema kuna mkandarasi alilipwa Sh bilioni tatu, kwa ajili ya kujenga maghala ya kuhifadhia tumbaku, lakini alijenga maghala mabovu ambayo hayafai. Fatuma alisema kuna ukaguzi ulifanyika, ukabaini hakuna utunzaji mzuri wa vitabu vya hesabu za pembejeo na wakulima hawakupewa mbolea badala yake walikatwa Sh bilioni 1.5.

Mbunge alia Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba alisema Taarifa ya Ukaguzi ya Mkoa wa Tabora imebainisha kuwa, viongozi wa vyama vya ushirika ni wezi na hufanya kazi kwa ubadhirifu.

Alisema ni vyema waliohusika na wizi wa mabilioni hayo ya fedha, wapelekwe mahakamani mara moja ili haki itendeke. Ahadi ya Kinana Akijibu malalamiko ya wakulima hao, Kinana alisema kilio cha wakulima wa tumbaku atakifikisha kwa Rais Kikwete, ili achukue hatua zaidi za kisheria.

Alisema kuna uozo wa kutupwa kwenye sekta ya tumbaku na amevitaka vyama vya ushirika kuwa tayari kubeba lawama za wakulima.HABARILEO

Post a Comment

 
Top