0
MAKALA
 Ikiwa wewe ni mwajiriwa mpya au ni mkongwe katika ajira, inabidi utambue kuwa kuna baadhi ya makosa hutakiwi kuyafanya mahali pa kazi kwa ajili ya mustakabali wako.
Makosa unayoyafanya leo yanaweza kukugharimu katika maisha yako yote ya ajira. Ukweli ni kuwa kuna makosa mengi tunayofanya katika maeneo ya kazi pasina sisi wenyewe kutambua.
Kosa la kwanza ni kuwa na tabia ya kulalamikalalamika mara kwa mara kuhusu kazi na kukosoa kwa uwazi mipango na sera mbalimbali za ofisi.
Mshahara mdogo, wingi wa kazi na matatizo mengine ni mambo yaliyopo katika ofisi nyingi. Inawezekana mabosi wasijali matatizo yako, lakini njia bora ya kuleta mabadiliko ni kuwa na subira na kufuata taratibu zilizopo.
Badala ya kulalamika na kuongea ovyo, waone mabosi na kuwafikishia malalamiko yako. Kulalamika na kuongea ovyo kutaharibu taswira yako kwa watawala na wanaweza kujenga chuki dhidi yako.
Epuka malumbano na mizozo na bosi wako au utawala wa kampuni. Ikiwa bosi wako amekutukana au kukufokea bila ya sababu usimjibu bali chukua hatua kwa mujibu wa kanuni na taratibu za kiofisi.
Bosi wako ana uwezo wa kukufanya upige hatua mbele au ubaki mahali ulipo. Uhusiano wowote mbaya kati yako na bosi wako utakuathiri zaidi wewe kuliko yeye.
Mchukulie bosi wako kama mshirika wako katika kazi na si adui. Hata kama unamchukia si lazima umwonyeshe.
Ni kosa kubwa kutokuchangamkia fursa zinazopatikana ndani na nje ya ofisi. Kila mara changamkia fursa zinazoweza kukuvusha kutoka hatua moja kwenda nyingine.
Onyesha dhamira kuwa unaweza kushika madaraka kama ukipewa na onyesha kuwa unafanya kazi ili upande cheo. Waulize mabosi nini unatakiwa ufanye ili uende hatua moja mbele na fanyia kazi ushauri utakaopewa ili kuboresha utendaji wako. Waajiri wengi hupenda watu walio makini katika kazi na wenye dhamira ya maendeleo.
Chunga muda wako unapokuwa ofisini. Matumizi mabaya ya muda yanaweza kukugharimu. Umeajiriwa ili kufanya kazi na siyo kuzurura ovyo au kupoteza muda katika mitandao ya kijamii au kutumia simu.
Kuna kesi kadhaa za watu waliowahi kufukuzwa kazi kutokana na matumizi mabaya ya kompyuta na simu mahali pa kazi.
Kuahidi mambo ambayo huna uwezo wa kuyatekeleza pia ni kosa linaloweza kukugharimu. Kuwa mkweli na ikibidi kataa kuchukua majukumu ya ziada ikiwa hutoweza kuyafanya kwa ufanisi.
Epuka kujivika vyeo ambavyo siyo vyako. Baadhi ya watu hujifanya mabosi wa ofisi wakati siyo kweli. Tambua majukumu yako na usivuke mipaka kwani ukifanya hivyo utakuwa unajitafutia matatizo ya bure.
Kosa lingine ni ile tabia iliyojengeka ya baadhi ya wafanyakazi kufanya yale tu waliyoambiwa. Hawa hawawezi kufanya majukumu ya ziada.
Daima jitahidi kuvuka malengo na kuweka rekodi mbalimbali za ufanisi kazini, kwani hayo ndiyo mambo yatakayokujenga katika maisha yako ya ajira.
Kosa lingine kubwa kwa wafanyakazi wengi ni kushindwa kujifunza kutokana na makosa yao. Muungwana daima haumwi na nyoka mara mbili kwenye shimo moja. Jifunze kutokana na makosa yako, boresha utendaji wako na pambana na changamoto zinazokukabili.MWANANCHI

Post a Comment

 
Top