Mtoto Samir mkazi wa mtaa wa Langoni kata ya Miembeni,akiwa amefungwa
kamba katika mguu wake wa kushoto huku upande mwingine ukiwa umefungwa
katika chuma kizito kilichopo jirani na mlango.
Na Dixon Busagaga
MTOTO Samir anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka minne hadi mitano
mkazi wa mtaa wa Langoni katika manispaa ya Moshi, amejikuta katika
wakati mgumu kutokana na tabia ya bibi yake kumfunga kamba katika mguu
wake kwa lengo la kumzuia asiende kucheza mbali na nyumbani kwao.
Tukio hilo limetokea hivi karibuni katika eneo hilo ambapo bibi huyo
ambaye jina lake halikufahamika mara moja alikutwa akiwa amemfunga
kamba ya kudu mjukuu wake huyo katika mguu wa kushoto huku sehemu
nyingine ikiwa imefungwa katika chuma kizito.
Kwa mujibu wa majirani walisema bibi huyo amekuwa akimfunga mtoto huyo
mara kwa mara kwa zaidi ya nusu saa hasa nyakati ambazo bibi huyo
amekuwa akifanya shughuli zake za usafi wa ndani pamoja na kufua.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina,majirani hao wamesema
imekuwa ni kawaida kwa bibi huyo ambaye anaishi na wajukuu zake
kumfanyia kitendo hicho mtoto huyo huku akimzuia kucheza na wenzake wa
nyumba za jirani.
“Sisi hiyo hali mbona tumeizoea mara kwa mara Samir akienda kucheza na
wenzake huko mtaani,bibi yake akimkuta huko anamkamata na kisha
kumfunga kwenye hilo chuma lililoko hapo mlangoni kwa zaidi hata ya
nusu saa”alisema mmoja wa majirani.
Akizungumza tukio hilo Bibi huyo ambaye anakadiriwa kuwa na miaka
zaidi ya 60 alikiri kumfunga mtotot huyo kwa madai kuwa amekuwa mtundu
kupita kiasi na kwamba ametumia mbinu hiyo ili kumdhibiti asitoroke
nyumbani.
“Hapa nyumbani naishi na wajukuu zangu ,wengine wako mashuleni na
wengine wako kazini ambao ni wazazi wa huyu Samir,mmoja anafanya kazi
Arusha,mwingine yuko hapo mjini(Moshi)sasa sina mtu wa kunisadia
kumwangalia huyu mtoto”alisema Bibi huyo.
Alisema analazimika kumfunga kamba mtoto Samir kutokana na kuwa na
tabia ya kwenda kuzurura katika nyumba za watu huku wakati mwingine
huenda kucheza mbali na nyumbani jambo ambalo humpa shida kumpata kwa
urahisi.
“Wakati mwingine nashikwa na hasira kumpiga siwezi hivyo naamua
kumfunga kamba hapa mlangoni…watu wote si wazuri kumruhusu kuingia
kila nyumba huko atafundishwa mambo mabaya ndio sababu nafanya
hivi.”alisema Bibi huyo.
Mmoja wa wazazi walioshuhudia tukio hilo walisema wazazi wengi
wamekuwa wakikosea kuwaacha watoto wao walelewe na bibi zao hali
inayochangia kuwepo kwa vitendo vya ukiukaji wa hali ya watoto na
kibinadamu kama ilivyotokea kwa mtoto huyo.
“Wazazi tumekuwa bize sana na shughuli za utafutaji ,hali hii
inapelekea majukumu ya kulea watoto kuiacha kwa wasichana wa kazi na
hata mama zetu kama ilivyo kwa familia hii ,sasa suala hili pia wakati
mwingine linachangia makuzi mabovu kwa watoto”alisema Juma Nzota.
Post a Comment