Na Ibrahim Yamola,
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ametoa
ruksa kwa wanachama wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kufanya mikutano yao nchi nzima.
Pinda alizungumza jana wakati akifunga maonyesho
ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwenye Viwanja vya
Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, alisema yaliyotokea bungeni yanaweza
kumalizika kwa kukaa meza moja ya majadiliano.
“Yale mambo ya bungeni yanaweza kumalizika na
tukaendelea kama ambavyo ilikuwa katika majadiliano ya kutengeneza
kanuni. Tulikuwa tukishindana kwa kukaa meza moja na kumalizana, kisha
tunaendelea sasa hili tumeshindwa nini?” alihoji Pinda
Alisema: “Walitoka bungeni na kusema watazunguka
nchi nzima, nasema wazunguke tu kuwaeleza wananchi na sisi hatutashindwa
kuzunguka kwani hoja tunazo.”
Waziri Mkuu Pinda alitumia nafasi hiyo kuelezea
kauli aliyoitoa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na
Bunge), William Lukuvi kwenye Kanisa la Methodist kwamba hoja ya
serikali tatu ikipita inaweza kulifanya jeshi kuchukua madaraka.
Alisema nilimpigia simu nikamweleza: “Rudi mara moja ueleze kilichotokea huko na nafikiri mlimsikia alichokisema.”
Lukuvi akitoa ufafanuzi bungeni bila ya kuwapo kwa
Ukawa alisema: “Nayasema yote haya kwa kuwa naamini huo ndio msimamo
wangu na utakuwa msimamo ambao wakati wote utaendelea kuwa hivyo na
ninawataka ndugu zangu kuacha unafiki.”
Kutokana na kauli hizo, Ukawa inayoundwa na vyama
vya Chadema, CUF, DP na NCCR-Mageuzi na wajumbe 25 kutoka kundi la 201
walitoka bungeni Jumatano wiki hii na kuahidi kuzunguka nchi nzima
kufanya mikutano ya hadhara kuwaleza wananchi kilichotokea.MWANANCHI
Post a Comment