Mbunge
wa Mfenesini (CCM), Suleiman Nassib Omar akiweka saini baada ya Mbunge
wa Nzega, Dk Hamisi Kigwangala (kushoto) kuanza kukusanya saini za
wabunge kwenye ukumbi wa bunge jana akitafuta kuungwa mkono katika hoja
ya kutokuwa na imani na Spika wa Bunge, Anne Makinda.PICHA NA EDWIN
MJWAHUZI
Dodoma:
Spika
wa Bunge, Anne Makinda amesema hatishwi na mchakato wa kumng’oa katika
nafasi yake ambao umeanzishwa na Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalla
kutokana na tuhuma za kukiuka kanuni za Bunge.
Kadhalika
Spika Makinda amepuuza hoja za Dk Kigwangalla akisema kuwa yeye
hajavunja kanuni yoyote, lakini akaweka bayana kuwa mbunge huyo wa Nzega
ana haki kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kuendelea na kile anachokifanya.
“Kanuni
si zinamruhusu, utaratibu upo kwenye kanuni za Bunge kwa hiyo aendelee
na mchakato lakini mimi ninachosema sitetereki maana hakuna kanuni
yoyote ambayo nimeivunja,” alisema Makinda katika mahojiano maalumu na
Mwananchi ofisini kwake jana.
Wakati
Spika akitoa kauli hiyo, jana, Dk Kigwangalla alianza harakati zake za
kukusanya saini za wabunge, akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya
kutokuwa na imani naye kwa madai kwamba amekuwa akikiuka kanuni.
Miongoni
mwa madai ya Dk Kigwangalla ni hatua ya Makinda kufanya uteuzi wa
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Bajeti, tofauti na kanuni zinazotaja wenyeviti kuchaguliwa na
wajumbe wa kamati.
Hoja
nyingine ni kamati hiyo ya bajeti kulipwa posho ya Sh430,000 wakati
wajumbe wa kamati nyingine wamekuwa wakipewa Sh130,000 pamoja na kumteua
Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba kuingia katika kamati hiyo ya
bajeti wakati mbunge huyo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu.
Jana
Dk Kigwangalla aliwasilisha hoja yake kwa Katibu wa Bunge na kuongeza
madai mapya yakiwamo ya kuagiza kwa mabavu majedwali ya mabadiliko ya
sheria kwenda kwenye kamati ya bajeti, kuvunja masharti ya kanuni ya 48
inayotoa maelekezo ya namna ya kuwasilisha na kujadili jambo la dharura
na kutumia madaraka yake vibaya kwa kuvunja masharti ya Sheria ya The
National Assembly (Administration) Act (Cap.115) ya mwaka 2008.
Makinda
akijibu hoja hizo jana alisema alifanya uteuzi wa Chenge kuongoza
Kamati ya Bajeti kwa sababu kamati hiyo ni mpya na haikuwapo katika
kamati za awali, hivyo ni wazo ambalo lilitokana na mawazo ya Bunge la
sasa.
“Tulikuwa
tunafikiria jinsi Bunge linavyoweza kuisadia Serikali ipate vyanzo
vipya vya mapato. Kwa hiyo tumehitimisha wazo hili kwa kuamua kuwa na
Kamati ya Bajeti. Kamati hii haikuwapo na wala utaratibu wake wa
kikanuni haukuwapo. Niliamua na kanuni zinanipa uwezo huo kwamba niteue
mtu ambaye ninaamini anaweza kuisimamia katika hatua za mwanzo ili tuone
uzoefu utatufikisha wapi,” alisema Makinda na kuongeza:
“Kamati
hii hata Serikali ilikuwa haikubaliani na sisi, lakini katika muda
mfupi wa utendaji wake umefanya kazi kubwa na kama tusingekuwa na Mzee
Chenge ambaye ni mzoefu na anafahamu vizuri utendaji wa Serikali basi
tungeshindwa na mimi siko tayari kuanzisha kitu halafu nikashindwa”.
Kuhusu
posho, Spika aliungana na kauli ya Katibu wa Bunge, Dk Thomas
Kashililah kwamba si wakati wote Kamati ya Bajeti imekuwa ikipewa malipo
zaidi, bali ni pale tu wanapofanya kazi nje ya siku na saa za kazi tena
kwa kibali chake.
“Lazima
walete maombi na waeleze kwa nini wanapaswa kufanya kazi kwa muda wa
ziada au siku za mapumziko na mimi nikisharidhia basi wanalipwa mara
mbili ya viwango vya kawaida na hiyo ni kwa mujibu wa taratibu na Kanuni
zetu,” alisema.Kadhalika alizungumzia
suala la wabunge wengine kuteuliwa kuingia kwenye kamati ambazo si zao
ambapo alisema, suala hilo pia ni la kawaida kwani hata katika mjadala
unaoendelea wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ameongeza wajumbe wa
ziada.
“Ninafanya
hivyo kupanua wigo wa mjadala na mara nyingi kwa mfano kwenye kamati
yetu ya Katiba nimeongeza wabunge wenye uelewa wa masuala ya sheria ili
watusadie kufanya uchambuzi, maana unaweza kukuta kwenye kamati, watu
wenye utaalamu kuhusu suala husika ni wachache. Kwa hiyo siyo kosa kwa
mujibu wa Kanuni zetu,” alisema Makinda.
Kwa
upande wake Dk. Kingwangalla jana alikuwa akiendelea na ukusanyaji wa
saini za wabunge huku akisema kuwa amewasilisha kwa Katibu wa Bunge
kusudio la kupeleka bungeni hoja yake.
Ukusanyaji
wa saini ulifanywa kwa kupitia fomu maalumu na kutoa taarifa kwamba
wabunge wa CUF na NCCR-Mageuzi, wote wameshasaini katika fomu hizo.
Akizungumza
jana katika viwanja vya Bunge, Dk Kigwangallah, alisema wabunge wa
Chadema, walimweleza kuwa watafanya hivyo baada ya kukutana katika kikao
cha pamoja.
Hata
hivyo Kiongozi wa Upinzani Bungeni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe alikiri kusikia taarifa hizo lakini akasema walikuwa bado
hawajaketi kama kambi ili kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu suala hilo.
Jana
asubuhi wakati wa kipindi cha maswali na majibu, Dk. Kingwangalla
alionekana akipita katika baadhi ya meza za wabunge akiwashawishi
kusaini fomu za kumuunga mkono.
Hadi jana mchana wabunge wa CCM, na CUF wapatao 30 tayari walikuwa wamesaini fomu hizo, wakimuunga mkono mbunge huyo.
Alipoulizwa
ulazima wa kukusanya saini za wabunge wakati kanuni hazimtaki kufanya
hivyo alisema, hilo linamwezesha kujua nguvu aliyonayo katika kumuunga
mkono kuhusiana na suala hilo.
Hoja zake Katika
taarifa ya kusudio lake ambalo Mwananchi imebahatika kuliona, Dk.
Kingwangalla alisema uteuzi wa Serukamba ni kinyume na masharti ya
kanuni ya 116(3) na (4).
Alisema
Juni 27, 2013, wakati wa kutunga sheria ya fedha, Spika aliagiza kwa
mabavu kuwa wabunge wote wenye majedwali ya mabadiliko waende kwenye
kamati ya bajeti.
“Uamuzi
huu wa Spika ni wa kidikteta na unapingana na masharti ya kanuni ya 88
ya kanuni za kudumu za Bunge ambapo kwa ufupi ni kwamba majedwali ya
mabadiliko hujadiliwa bungeni wakati wa kamati ya Bunge zima na
huamuliwa kukubaliwa ama kukataliwa na Bunge zima na si kamati yoyote ya
Bunge,” alisema.
Alisema
hatua hiyo ya kuipa mamlaka makubwa kamati hiyo ni kuondoa mantiki ya
uwepo wa Bunge lilopewa mamlaka ya kutunga sheria zote za nchi na Katiba
ibara ya 63 (3) ( c) na (d ).
Pia
alisema Spika Makinda amekuwa wa kwanza kuvunja masharti ya kanuni
anazopaswa kuzitilia nguvu kama anavyoelekezwa na kanuni ya 5 (2).
Amevunja pia kanuni na hivyo anastahili kuhukumiwa na kuadhibiwa kwa
mujibu wa masharti ya kanuni hizi ili kukidhi masharti ya Ibara ya 84
(7) (d) ya katiba ya kumwondoa madarakani.
Alitoa
mfano wa hoja ya dharura iliyotolewa wakati MV Skagit ilipozama Julai
18, 2012 na siku zilipowasilishwa hoja mbili zinazohusiana na mauaji ya
kwenye vurugu zinazohusu migogoro baina ya jamii za wakulima na wafugaji
na wanyang’anyi wa mali na unyanyasaji wa wafugaji unaofanywa kwenye
operesheni tokomeza ujangili.
Katika
kuhitimisha taarifa hiyo, Dk Kingwangalla alisema: “Ni maoni yangu
binafsi na ya wabunge wengi wanaoniunga mkono kuwa Spika wa Bunge Anne
Makinda apumzishwe kazi kwa tuhuma nilizozitaja hapo juu.”
|
Post a Comment