Mshambuliaji wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Cedric Bakambu, amekamilisha kuhamia klabu ya Beijing Guoan ya China, na kuwa mchezaji ghali zaidi kutoka Afrika kwa sasa.
Klabu hiyo ya ligi kuu ya soka nchini Uchina, haijatangaza hadharani kiasi cha pesa alizonunuliwa mwanakandanda huyo mwenye umri wa miaka 26. Lakini imesema tu ni zaidi ya dola milioni 90 za Marekani.
Kiwango hicho kinashinda kile cha dola milioni 77 ambazo zilitolewa kumnunua mchezaji wa Arsenal Pierre- Emerick Aubameyang wa Gabon mwezi uliopita.
Duru zimefichua kuwa, Bakambu amesaini mkataba wa miaka minne.
Beijing Guoan, ambayo ilimaliza ya 9 katika msimamo wa ligi kuu ya China yenye timu 16 ilikuwa imetarajia kulipa kiasi kidogo cha pesa kwa mchezaji huyo aliyeondoka Villareal ya Uhispania mwezi Januari, baada ya kufikishwa kwa kiwango cha dola milioni 50 cha kumfungua kutoka katika mkataba wake.
Klabu hiyo ya Uchina, ilijaribu kuwashawishi maafisa nchini DRC kwamba hakukuwa na haja ya kulipa mara dufu ya kiasi hicho kama inavyohitajika na sheria za ushuru nchini China, hasa kwa sababu mchezaji huyo alikuwa ajenti huru - hakuwa kwenye mkataba wowote.
Hata ingawa timu ya Beijing Guoan ilishindwa katika hili, walifaulu kupunguza kiwango hicho cha kodi kinachohitajika kutoka Dola milioni 50 hadi Dola Milioni 40m - na kuokoa Dola milioni 10.
Mwaka jana, FA ya China iliamua kuwa, vilabu vya kandanda nchini humo vinafaa kulipa asilimia 100% ya ushuru katika kila mwanasoka anayesajiliwa nchini humo, katika juhudi za kukabiliana na matumizi mabaya ya pesa, huku pesa za ziada zikielekezwa kuboresha mchezo huo mashinani.
Licha ya kukosa uhamisho rasmi, Bakambu alianza kufanya mazoezi na wanasoka wa timu yake ya Ureno, mwezi Januari - huku klabu hiyo ikichapisha picha ya mshambuliaji huyo akiwa mazoezini.
Bakambu, mchezaji pekee wa kandanda barani Afrika kunyakua tuzo ya mchezaji bora wa mwezi katika Ligi Kuu ya Uhispania, alikuwa miongoni mwa wafungaji mabao bora La Liga ambapo alikuwa amefunga mabao 9 kufikia wakati alipokuwa anaondoka Villareal.
Alijiunga na klabu hiyo ya Uhispania mwaka 2015 kutokea timu ya Uturuki Bursaspor, ambapo alifunga jumla ya mabao 21, msimu mmoja tu alipoichezea klabu hiyo.
Bakambu ni mzaliwa wa Ufaransa na alichezea timu ya taifa ya Ufaransa ya vijana kabla ya kubadilisha uamuzi na kuamua kuichezea DRC mwaka 2015.
Amefungia timu ya taifa ya DRC mabao saba.
Post a Comment