Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongea na wananchi wa Kata ya Chiungutwa, Wilayani Masasi, akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku tatu, Mkoani Mtwara Februari 27, 2018.
Na. Mwandishi Wetu, Masasi.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema viongozi wa Vyama vya Ushirika waliokula fedha za wakulima wa korosho wilayani Masasi wazirudishe na wakishindwa mali zao zikiwemo nyumba zitauzwa ili kufidia.
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Gelasius Byakanwa ahakikishe anawasaka viongozi wa chama Ushirika cha Msingi cha Nanyindwa wilayani Masasi ambao wamekula fedha za wakulima na kisha kutoroka.
Amesema viongozi wa vyama vya Ushirika katika wilaya hiyo si waaminifu, ambapo mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya sh. bilioni 2.3 za wakulima ziliibiwa na viongozi hao, ambapo mwaka 2017/2018 sh. bilioni 1.7 zimeibiwa.
Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo Jumatatu, Februari 26 2018 alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi pamoja na watumishi wa wilaya akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara.
Alisema viongozi wa Ushirika wa Nanyindwa ambao wametoroka ni Michael Mkali, Yusuph Mataula, ambapo alimuagiza Bw. Byakanwa kuwasaka na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola ili waweze kuchukuliwa hatua zinazostahili.
Pia Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuvichunguza vyama vya Msingi katika maeneo na wakikuta kuna kiongozi amekula fedha za wakulima wamkamate na kumchukulia hatua za kisheria.
Alisema wakati wa watu kuomba kuchaguliwa kuongoza vyama vya Ushirika kwa lengo la kujitajirisha umepita na Serikali imedhamilia inawasimamia wakulima wa mazao mbalimbali nchini wakiwemo wa korosho ili kuhakikisha nao wananufaika.
Waziri Mkuu alisema vyama vya Ushirika wilaya hiyo vinaongoza kwa ubadhilifu wa fedha za wakulima ambapo wiki iliyopita Bw. Byakanwa aliwakamata viongozi 36 wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) wilayani Masasi.
Viongozi hao ambao ni wenyeviti na makatibu wanakabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za wakulima wa korosho ambazo ni zaidi ya sh bilioni 2.3, ambazo ni malipo ya zao hilo kwa msimu wa ununuzi 2016/2017 na 2017/18.
Alisema mbali na wafanyabiasharahao, pia Meneja wa benki ya NMB tawi la Masasi, Aidan Msuya anaye alikamatwa kwa tuhuma za kufanya muamala wa fedha za malipo ya wakulima sh milioni 45 kwa zaidi ya mara 11 kwa siku moja.
Waziri Mkuu alimpongeza Bw. Byakanwa kwa hatua alizozichukua dhidi ya viongozi hao na kumuagiza ahakikishe viongozi wote waliosababisha ubadhirifu huo wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Post a Comment