Na Mwandishi Wetu, Songosongo.
Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa inadaiwa shilingi 143,010,138.44 kama gawio la asilimia ishirini (20%) na kijiji c ha Songosongo kutoka katika malipo ya tozo ya huduma ya asilimia 0.3 ambayo halmashauri hiyo hulipwa na makampuni yanayofanya shughuli za uziduaji wa gesi asilia kijijini hapo.
Hayo yamefahamika kupitia kampeni ya kuhimiza uwazi na uwajibikaji katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato inayofanyika katika wilaya ya Kilwa kuanzia mwaka 2015.
Kampeni hiyo ni sehemu ya mafunzo ya utambuaji haki stahiki kwa kuangalia taarifa zilizopo yaliyotolewa na Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Lindi (LANGO) kwa ufadhili wa shirika la Oxfam Tanzania.
Katika kikao cha majadiliano na Waraghbishi na baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji na kata ya Songosongo kulionekana mapungufu makubwa kuhusu kiasi cha fedha kilicholetwa kijijini hapo kutoka halmashauri ikilinganishwa na kiasi cha fedha ambacho halmashauri imeshapokea kutoka kwa makampuni hayo ya uziduaji wa gesi asilia.
Baada ya kubaini mapiungufu hayo serikali ya kijiji kwa kushirikiana na waraghbishi wametengeneza Mpango Kazi wa kufuatilia kiasi hicho cha fedha kilichopaswa kupelekwa kijijini hapo kama gawio la asilimia 20 na halmashauri. Aidha katika mpango kazi huo uliitafadhalisha halmashauri kusema kiasi hicho cha fedha kitalipwa lini katika kijiji hicho ili waendeleze mipango yao ya maendeleo.
Hata hivyo taarifa zilizopatikana baadae katika mkutano huo zilionesha kwamba kumekuwa na ugumu kwa halmashauri kueleza waziwazi kuhusu pato hilo na nini kinafanyika kwa mujibu wa sheria zilizopo.
“Hakika haikuwa kazi rahisi kwa serikali ya kijiji na wananchi wa Songosongo kukutana na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ili kuulizia deni la kiasi cha fedha kilichopaswa kuletwa kijiji lakini haikufanyika hivyo na kuomba taarifa rasmi ikijumuisha mikakati ya kulipa fedha hizo kwa manufaa ya wananchi wa Songosongo” alisema Andrew Hassan mmojawapo wa waraghbishi mahiri waliounda timu kazi ya kwenda Halmashauri.
Mjumbe mwingine katika kamati iliyoenda kumwona DED kuzungumza kuhusu tozo hilo Salma Ahmed alisema alisema kwamba wanandaa ziara nyingine kwani wanakijua wanchokitafuta baada ya kupewa elimu na asasi ya Lango.
“Kwa kweli tunaishukuru sana asasi ya LANGO na shirika la Oxfam Tanzania kwa kutujengea uwezo na kujiamini hadi kuunda timu iliyokwenda kuonana na Mkurugenzi Mtendaji katika jitihada za kufuatilia haki na stahiki yetu wananchi wa Songosongo” alinena Salma Ahmed ambaye ni Katibu wa waraghbishi wa kijiji cha Songosongo .
Kijiji cha Songosongo kimebarikiwa kuwa na gesi asilia ambayo pia inasaidia ufuaji wa umeme unaotumiwa katika gridi ya taifa.
Post a Comment