Mabosi wa Yanga wanaendelea na mchakato wa kukamilisha taratibu za kumleta nchini Mguinea, Bensua Da Silva lakini kuna mwingine pia atatua kutoka Sierra Leone.Mabosi wa Yanga hawataki kufanya mambo kwa kubahatisha kwani wanaleta wachezaji hao kuja kuwajaribu na kama watakuwa moto kama mawakala wao wanavyojitamba, basi wanaweza kubaki Jangwani wote na waliopo sasa wakaliwa vichwa.
Wa kwanza kupigwa chini ni Donald Ngoma ambaye kocha, George Lwandamina, hataki hata kusikia jina lake. Mchezaji mwingine mpya wanayemtaka ni Msierra Leone, Badara Kella ambaye kwa mujibu wa mitandao ya kimataifa hajafikisha miaka 30.
Wanachotaka Yanga ni kuwa na idadi ya mastraika watatu mpaka wanne kuwapima kwa pamoja kisha kufanya maamuzi ya yupi achukuliwe kabla ya kukamilisha kutuma orodha ya majina ya wachezaji watakaoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Kella ameshawaridhisha mabosi wa Yanga, lakini nao hawataki kubahatisha wanamleta nchini kuja kuangaliwa kwa jicho la ufundi na benchi lao la ufundi chini ya Lwandamina.
Lwandamina anatumia sakata la Ngoma kuboresha nidhamu ya wachezaji mastaa wanaoleta usumbufu katika timu hiyo ambapo amewaambia viongozi kwamba wachezaji wote watakaofuzu lazima wakubaliane na masharti ya kufanya tathmini ya utendaji wao kila baada ya miezi sita.
Mbali na Kella pia kuna uhakika kwamba bado kuna mshambuliaji mmoja wa Nigeria ambaye ataungana na Silva na Kelva.
Post a Comment