Ni miaka minne leo tangu kuanza kwa vita vya kiraia nchini Sudan kusini.
Ghasia hizo zimekuwa wimbi jeusi lililo zima matumaini yaliokuwepo yaliotokana na uhuru wa kujitenga na serikali ya Khartoum mnamo mwaka 2011.
Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni wengine wameachwa bila ya makaazi.
Vita vilianza Sudan kusini baada ya rais Salva Kiir kumtuhumu aliyekuwa makamu wa rais Riek Machar kwa kupanga mapinduzi.
Kabila la Machar - Nuer - ambalo ni la pili kwa ukubwa katika nchi hiyo baada ya kabila la Dinka la rais Salva Kiir - lilitazama mzozo huo kama mauaji ya kimbari dhidi yao.
- Waasi watangaza vita dhidi ya serikali Sudan Kusini
- Salva Kiir aitisha mazungumzo ya kitaifa
- Amani yaanza kutengamaa Sudan Kusini
Wanachama wa kamisheni ya haki za binaadamu katika Umoja wamataifa nchini Sudan Kusini leo wanatoa ripoti ya utafiti wao wa siku mbili walioufanya katika jimbo lililopo kaskazini magharibi la Wau.
Wamekwenda kukusanya na kuhifadhi ushahidi wa ukiukaji wa aina yoyote na unyanyasaji wa haki za binaadamu na uhalifu unaohusiana na hilo.
Maisha hivi sasa kwa raia
Hivi leo bado hali ni ya kuogofya. Ni mvua kubwa tu ya msimu ndiyo inayositisha mapigano, angalau kwa muda.
Taifa limesambaratika - huku Umoja wamataifa ukionya kuwepo hatari ya kufanyika mauaji ya kimbari.
Raia nchini humo wamekabiliwa na ubakaji, mauaji na katika baadhi ya maeneo - baa la njaa.
Miezi sita iliyopita, kuliitishwa msaada mkubwa kukabiliana na baa la njaa nchini.
Leo inakadiriwa raia milioni 4.8 bado hawapati chakula cha kutosha - ikiwa ni ongezeko la milioni 1.1 kutoka mwaka jana.
"Miaka minne tangu kuanza mzozo wa Sudan kusini, hali inazidi kuwa mbaya na matumaini ni finyu kwa hali kuimarika," amesema Rehana Zawar, Mkurugenzi wa shirika la wakimbizi Norway nchini Sudan kusini.
"Raia, wengi wao wanawake na watoto ndio waathiriwa wakuu wakati ghasia hizo zikiongezeka katika maeneo mengi ya nchi. Wakulima wanaogopa kushughulikia mazao yao, na wanawake wanakabiliwa na hatari ya kubakwa kila siku wanapokwenda kuteka maji na kukusanya kuni."
Uchumi umezorota. Jitihada za kuutatua mzozo zimeambulia patupu.
Wiki ijayo mazungumzo ya kutafuta kufikiwa makubaliano ya amani ambayo wengi wanayaona hayawezi kuokolewa - yanatarajiwa kufanyika katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa.
Lakini hakuna ishara ya vita hivyo vya kiraia kumalizika wakati wowote hivi karibuni.
Post a Comment