Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika cha RUNALI, Hassan Mpako
Na. Ahmad Mmow. Liwale
CHAMA kikuu cha ushirika cha RUNALI kinatarjia kujenga ghala la kutunzia mazao ya kilimo wilayani Ruangwa. Hayo yameelezwa disemba 10 na mwenyekiti wa chama hicho, Hassan Mpako katika kijiji cha Mikunya wilayani Liwale.
Mpako ambae aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mnada wa nane wa zao la korosho ambao disemba 10 ulifanyika katika kijiji hicho, alisema katika kukabiliana na Uhaba wa maghala, chama hicho kinakusudia kujenga ghala kubwa lenye uwezo wa kihifadhi takribani 10,000.
Alisema mpango huo upo katika hatua za awali. Ambapo tayari wamefanikiwa kupata kiwanja katika mji wa Ruangwa. Alibainisha kwamba kuna umuhimu mkubwa wa chama hicho kuwa na ghala lake badala ya kutegemea maghala ambayo hawana uhakika kama wanaweza kuwa nayo. Kwasababu wamiliki wanaweza kuwapa wawekezaji. “Kwa mfano yale maghala ya Lindi Farmers serikali inaweza kuyachukua nakuwapa wawekezaji wanaoweza kuendeleza kiwanda kile, kwahiyo matarajio yetu msimu ujao ghala hilo liweze kutumika,” alisema Mpako.
Aidha mwenyekiti huyo aliwatangazia vita wakulima walioazima magunia, lakini hawataki kurejesha. Alisema muda wowote kuanzia sasa chama hicho kitaanza zoezi la kuwasaka wakulima hao. Kwasababu wanasababisha upungufu wa magunia. Wakati korosho nyingi hazitolewi kwenye maghala ya vyama vya msingi kutokana na ukosefu wa magunia.
Kwa upande wake meneja mkuu wa chama hicho, Christopher Mwaya, alitoa wito kwa watendaji wa vyama vya msingi kuwa makini katika kuandaa taarifa za malipo ya wakulima ili kuepuka ucheleweshaji wa malipo. Huku pia akiwaasa wakulima kuacha kutumia akaunti za watu wengine. Alisema baadhi ya mambo yanayosababisha ucheleweshaji wa malipo ni uchanganyaji wa taarifa unaofanywa na baadhi ya wakulima. “Mkulima mwingine Jina aliloandika kwenye cheti ni tofauti na jina la kwenye akaunti yake,” alisema Mwaya.
Katika mnada huo bei ya juu ilikuwa shilingi 3,935. Wakati bei ya chini ilikuwa shilingi 3873.
Post a Comment