0
 Kaimu Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga (wa kwanza kulia kwa waliokaa) akishuhudia ufunguaji wa Zabuni ya Ujenzi wa mradi wa Umeme wa  Stiegler’s Gorge (MW 2100) uliofanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam. Katikati  ni  Mkurugenzi wa Idara  ya Manunuzi, Wizara ya Nishati, Armon Macachayo na wengine ni Viongozi Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati pamoja na watendaji  kutoka Kampuni mbalimbali. 
Viongozi Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati pamoja na watendaji kutoka kampuni mbalimbali zilizonunua zabuni ya Mradi wa Umeme wa Stiegler’s  Gorge wakiwa katika kikao cha ufunguaji wa Zabuni hizo jijini Dar es Salaam.



Zabuni ya Ujenzi wa Mradi wa kuzalisha Umeme kiasi cha MW 2100 kwa kutumia maporomoko ya maji katika Mto Rufiji (Stiegler's Gorge) imefunguliwa leo tarehe 27/11/2017 ambapo Kampuni 81 zilijitokeza kununua nyaraka za Zabuni hizo na kampuni Nne ndizo zilizorudisha nyaraka za zabuni husika. 

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ugavi ya Wizara ya Nishati, Armon Macachayo wakati wa kikao cha Zabuni hiyo kilichofanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dar es Salaam.

Macachayo alisema kuwa baada ya ufunguaji wa Zabuni husika, Zoezi linalofuta ni kufanyika kwa tathmini ili kupata Kampuni moja itakayokidhi vigezo vya kukabidhiwa mradi.

Zabuni hiyo ilitangazwa tarehe 30 Agosti, 2017 ambapo Serikali kupitia iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini, ilialika Taasisi Binafsi na Kampuni zenye uwezo kutoka ndani na nje ya nchi kujitokeza kuomba zabuni husika.

Akitoa taarifa za kutangazwa kwa Zabuni husika mwezi Agosti, 2017, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alisema kuwa Mkandarasi atakayepewa kazi ya kujenga mradi huo ni yule atakayeridhia kujenga mradi husika kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi na kusema kuwa kukamilika kwa mradi husika kutasaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme nchini.

Inatarajiwa kuwa, baada ya zoezi la tathmini na majadiliano ya mkataba wa ujenzi kukamilika, mwanzoni mwa mwezi Januari mshindi wa zabuni hiyo atakabidhiwa Mradi ili kuweza kuanza kazi ya ujenzi wa mradi mara moja.

Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga alishukuru kampuni zote zilizojitokeza kununua zabuni husika na kuwakaribisha kuwekeza katika miradi mingine ya uzalishaji Umeme.

Post a Comment

 
Top