0
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza akijibu maswali mbalimbali ya wabunge wakati wa mkutano wa tisa wa kikao cha nane cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Mjini Dodoma.
……………..

Na Lorietha Laurence-WHUSM,Dodoma.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana
Shonza ameeleza kuwa kazi kubwa ya kamati iliyoteuliwa na Dkt.
Mwakyembe ni kuainisha maeneo yatakayotumika wakati wa mashindano ya AFCON kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 yanayotarajiwa kufanyika
hapa nchini mapema mwaka 2019.

Naibu Waziri huyo, ameyasema hayo leo Bungeni Mjini Dodoma alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Singida Magharibi Mhe. Elibariki Kingu
aliyetaka kufahamu kama serikali imeteua mji mwingine tofauti na Jiji
la Dar es Salaam kwa ajili ya kuendesha mashindano hayo.

“Moja ya vigezo vya kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON ya vijana
chini ya umri wa miaka 17 ni kuwa na viwanja vyenye hadhi ya kimataifa
ndio maana haya mashindano yamechaguliwa kufanyika Jijini Dar es
Salaam” amesema Mhe. Shonza.

Aidha Mhe. Shonza amesema,mbali na kuwa na viwanja vyenye kukidhi
viwango vya kimataifa ni lazima mkoa husika uwe na hoteli za kisasa
ambazo zitatosheleza wageni mbalimbali watakaokuja kushuhudia
mashindano hayo kutoka nje na ndani ya nchi.

Tanzania kwa mara ya kwanza inakuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON ya vijana chini ya umri wa miaka 17 jambo ambalo ni fursa kubwa kwa nchi yetu kujitangaza kupitia sekta mbalimbali ikiwemo Maliasili na Utalii na hivyo kuisaidia katika kutangaza na kukuza uchumi wa nchi.

Post a Comment

 
Top