0
KINARA wa Muungano wa National Super Alliance (NASA) Raila Odinga ametangaza maandamano ya siku mbili kuanzia kesho


Akizungumza katika Kanisa Katoliki la St Peter’s Kiminini, Trans-Nzoia, Bw Odinga alisema maandamano hayo ya Jumanne na Jumatano yanalenga kushinikiza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufanya mageuzi kabla ya kuandaa uchaguzi wa urais wa marudio.

“Jumanne kutakuwa na maandamano, Jumatano pia tutaandamana na Alhamisi hakuna uchaguzi,” akasema Bw Odinga.
Maandamano hayo huenda yakatatiza maandalizi ya uchaguzi wa Oktoba 26 haswa katika ngome za NASA.
Bw Odinga wiki iliyopita alisema atatoa mwelekeo Oktoba 25 kuhusu hatua ambayo wafuasi wake watachukua wakati wa uchaguzi wa Alhamisi.
Kiongozi huyo wa Upinzani alisema maandamano ni haki ya kikatiba ya Wakenya na hivyo ‘waandamanaji hawafai kuadhibiwa kwa kupigwa risasi na polisi’.
Bw Raila alidai kuwa ana ushahidi wa kuonyesha kuwa uchaguzi wa Oktoba 26 umesheheni udanganyifu.
“Tuna ushahidi wa kuonyesha kuwa uchaguzi wa Alhamisi una dosari. Tayari magari ya polisi yanasafirisha karatasi za kura. Ukweli ni kwamba kiasi kikubwa cha kura zilichapishwa jijini Nairobi na wala si Dubai kama mnavyoelezwa,” Bw Odinga akawaambia waumini.
Alidai kuwa kujumuishwa kwa Bw Cyrus Jirongo katika karatasi za kura ni ithibati kwamba karatasi za kura zilichapishiwa hapa Kenya.
“Bw Jirongo alitangazwa na korti kuwa amefilisika, mbona IEBC ilimjumuisha katika karatasi ya kura? Walijumuisha wawaniaji wote wanane kwa sababu karatasi zilikuwa zimechapishwa na Jubilee jijini Nairobi,” akadai Bw Odinga.
Alisisitiza kuwa hatashiriki uchaguzi wa Alhamisi ambao utahusisha Rais Uhuru Kenyatta, Mohamed Abduba Dida, Dkt Ekuru Aukot, Bw Jirongo, Dkt Japhet Kaluyu, Prof Michael Wainaina na Joseph Nyagah.
“Uhuru hana mshindani, anashindana peke yake. Sisi tunahitaji uchaguzi ambapo Uhuru anashindana na Raila bali si uchaguzi wa mtu mmoja,” akasema Bw Odinga.

Chanzo: swahilihub

Post a Comment

 
Top