0
Na. Ahmad Mmow, Lindi.
KAULI MBIU waliyotunga wananchi wa mtaa wa Muungano kata ya Mnazimmoja inayotambulika kwa “TOFALI MOJA LINAJENGA” imeanza kutoa matunda. Baada ya wananchi hao kuanza ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja.
Wakizungumza na mwandishi wetu, shuleni hapo, baadhi ya walimu na wananchi walisema hawawezi kuendelea kusubiri serikali  wakati wanazo nguvu za kutosha na uwezo wakupunguza uhaba huo wa vyumba vya madarasa.
Mwalimu kiongozi wa shule ya msingi Muungano, Joyce Majumba alisema ushirikiano uliopo baina ya walimu, kamati ya shule na wananchi umechangia wananchi kuhamasika kuanza kujenga madarasa mawili na ofisi moja kupitia kauli mbiu ya “TOFALI MOJA LINAJENGA”. Mwalimu Majumba ambae shule yake ina walimu 9 na wanafunzi 645, alisema  inaupungufu wa madarasa 7 kati ya 14 yanayohitajika  kukidhi mahitaji.
“Wananchi wamehamasika zaidi baada ya mbunge wa jimbo la Lindi, mheshimiwa Hassan Kaunje kutuunga mkono kwa kuchangia tofali 500 na saruji mifuko 50. Mahusiano mazuri baina ya sisi walimu na kamati ya shule pamoja na wananchi ndio msingi wamafanikio yanayoweza kupatikana,” alisema Majumba.
Alisema madarasa hayo kupunguza tatizo hilo linalosababisha wanafunzi wa darasa la kwanza 147 kutumia chumba cha darasa kwa zamu, ambapo wanafunzi 82 wa darasa la pili wanasomea kwenye chumba kimoja. Wakati  idadi ya wanafunzi wanatakiwa kukaa kwenye chumba kimoja cha darasa ni 45 tu.
Mwalimu Majumba alisema licha ya vyumba vya madarasa lakini pia shule hiyo inakabiliwa na upungufu wa matundu ya vyoo. Japokuwa mahitaji halisi ni matundu 25, lakini shule hiyo inamatundu ya vyoo 9 tu.
Mwananchi Asha Chingolele,alisema wananchi na viongozi wao wamebaini kuwa matatizo yaliyopo katika mtaa wao yataondolewa na wao wenyewe. Bali wafadhili na serikali wawe waungaji  mkono juhudi zao. Asha aliahidi wananchi wataendelea kutatua changamoto zilizopo katika shule hiyo na mtaa wao kwa jumla. Kwasababu niwajibu wao kuhakikisha watoto wanapata elimu katika mazingira bora na maendeleo yanaletwa na wananchi wenyewe.
Maneno ya Asha yaliungwa mkono na mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, Juma Dadi aliyesema kampeni ya kuboresha miundombinu ya shule hiyo kupitia kauli mbiu ya “TOFALI MOJA LINAJENGA” ni endelevu.

Post a Comment

 
Top