0
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imefanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya kombe la Cosafa Castle baada ya muda mfupi uliopita kutoka sare ya kufungana bao 1-1 timu ya taifa ya Ushelisheli katika mchezo wake wa mwisho wa kundi A uliochezwa kwenye uwanja wa Moruleng huko Rusternburg, Afrika Kusini.
Ushelisheli ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza kupitia kwa Kelvin Perticots aliyefunga katika dakika ya 67 kabla ya Simon Happygod Msuva kuisawazishia Taifa Stars katika dakika ya 68.
Aidha Ushelisheli ililazimika kumaliza mchezo ikiwa pungufu baada ya Damien Balisson kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa mchezo mbaya.
Sare hiyo imeifanya Taifa Stars imalize hatua ya makundi ikiwa kileleni mwa kundi A baada ya kujikusanyia pointi tano. Nafasi ya pili imeshikwa na Angola yenye pointi tano pia baada ya leo kutoka sare ya bila kufungana na Malawi lakini inazidiwa na Taifa Stars kwa tofauti ya mabao ya kufunga.
Sasa Taifa Stars itavaana na wenyeji ambao pia ni mabingwa watetezi, Afrika Kusini kwenye mchezo wa robo fainali utakaochezwa Jumapili ya wiki hii.

Post a Comment

 
Top