0
Jumamosi Juni 24, 2017, Tanzania iliamua kuita barabara moja nchini humo jina V. Wanyama Street.
Hata hivyo, habari za barabara hiyo kubadilishwa kutoka Shekilango Road hadi Victor Wanyama Road zimepokelewa kwa hasira na Watanzania wengi.
Baadhi yao wanapendekeza wanasoka maarufu kutoka Tanzania kama Mbwana Samatta anayechezea Genk nchini Ubelgiji wapewe heshima hiyo.
Wengine wamesema ni aibu kubwa barabara hiyo kuitwa mtu ambaye si Mtanzania, huku wengine wakidai Tanzania imerogwa kwa kumuenzi Mkenya huyo anayelipwa na Spurs mshahara wa Sh9.2 milioni kila wiki.
Baada ya kupokea habari hizo, shabiki Rashid Kassa alisema, “Shekilango ya bongo au? Kwa lipi haswa? Jellah Mtagwa, Gibson Sembuli, Kitwana Manara, Leodgar Chillah Tenga, Abdallah 'king’ Kibaden, Said Nassor Mwamba Kizota, Hussein Amani Masha na wengine wengi ni wachezaji wa kibongo… sidhani kama wana mitaa ya majina yao kuwaenzi.”
Naye Nicodemus Girbert alisema, “Hivi wa Tanzania tumerogwa? Huyu mtu ana historia gani Tanzania? Acheni kujipendekeza banaa, na ni nani mwenye mamlaka ya kupanga majina…?”
“Huo ni upuuzi ametufanyia nini hadi apewe mtaa. Kwanini tusiwape wachezaji wetu. Acheni ulimbukeni,” alichemka David Ramadhani Chavaligino.
Joseph Gimonge alisema, “Huu ni ujinga wa juu. Kuna wachezaji wetu wamelifanyia taifa hili mambo makubwa hawana hata jina kwenye kitongoji achia mbali mtaa leo wanampa huyu Mkenya mtaa….”
Naye Juma Kidunda alidai ni muda tu kabla ya Victor Wanyama Road kubadilishwa. “Baada ya sikukuu ya Eid al-Fitr, hilo jina litatenguliwa, subirini mtaona.”
Mashabiki P Xtra Jalous na Simon Japhet waliona manufaa makubwa katika ziara ya Wanyama. “Wabongo mnapenda kulalamika sana. Ni dalili ya umasikini...kila kitu mnakitazama kwa mtazamo hasi. Jipe hata nafasi kidogo ya kutafakari,” alishauri P Xtra Jalous.
Naye Simon Japhet aliongeza, “Mimi naona ni sawa tu. Ujio wa Victor Wanyama ukiufuatilia kindani una manufaa hasa katika kuhamasisha mchezo wa soka nchini Tanzania kwani wachezaji wengi hasa wanaochipukia watapata chachu ya kutaka kufanikiwa… ameeleza sana mambo ya msingi na ametia moyo sana wachezaji wetu na amekuwa mzalendo kama Mwafrika mashariki mwenzetu. Sisi kama Watanzania tusipende kubeza vitu ambavyo vinaweza kusaidia hapo mbeleni.
Hatua ya mtaa kupewa jina lake ni kama tumempa deni ambalo huwezi kujua kama ataweza kulipa. Hatujui iwapo anaweza kuwa balozi mzuri wa nchi yetu hata akashawishi baadhi ya wachezaji wenzake kuja kuitembelea Tanzania.”
Nahodha wa Kenya, Wanyama alitunukiwa heshima hiyo baada ya kuhudhuria mashindano ya Ndondo Cup mtaani Ubongo jijini Dar es Salaam.
Barabara hiyo inayoelekea katika uwanja wa Kinesi Ground, ilizinduliwa rasmi na Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob kabla ya mechi kati ya timu za Faru Jeuri na Kauzu mnamo Jumamosi.
Kiungo huyu aliyesaidia Spurs kumaliza Ligi Kuu ya Uingereza katika nafasi ya pili nyuma ya Chelsea, alikuwa Tanzania kwa likizo ya wiki nzima.
Heshima ya Wanyama kuitwa barabara hiyo iliwasili saa chache baada ya kushinda taji la mwanaspoti mwenye ushawishi mkubwa katika tuzo za mitandao ya kijamii nchini Kenya (SOMA).
Alibwaga bingwa wa marathon katika michezo ya Olimpiki, Eliud Kipchoge, mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 800 David Rudisha, seta shupavu Jane Wacu na nyota wa raga Biko Adema.
Wanyama anatarajiwa kuwa katika safari ya Spurs nchini Marekani mwezi ujao ambapo watacheza dhidi ya PSG, AS Roma na Manchester City katika mashindano ya International Champions Cup.  

Chanzo:swahilihub

Post a Comment

 
Top