Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa, Mbunge wa Singida Mashariki kupitia tiketi ya Chadema, Tundu Lissu alikamatwa baada kutolewa kwa amri ya kufanyika hivyo kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum (ZCO).
MKUU wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Wilaya (OCCID), Yustino Mgonja ameeleza hayo leo mbele ya Hakimu MKazi Godfrey Mwambapa wakati akitoa ushahidi wake kama shahidi wa nne katika kesi ya kutumia lugha ya uchochezi inayomkabili Lissu ilipokuja kusikilizwa.
Akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi, Mgonja amedai kuwa Juni 28, mwaka jana, ZCO Wambura alimpa maelekezo ya kumkamata Lissu kwa kosa la kutoa lugha za uchochezi katika Viwanja vya mahakama hiyo.
Amedai, Juni 29 mwaka jana, majira ya mchana alienda nyumbani kwa Lissu maeneo ya Tegeta wilayani Kinondoni ambapo alimkamata na kumfikisha katika Ofisi za ZCO na kumkabidhi.
Alidai kuwa, alipewa amri na ZCO kumkamata Lissu na alifanya hivyo licha ya kuwa hakuwa na hati ya ukamataji kwa kuwa mamlaka yalikuwa yanamruhusu kufanya hivyo na kuwa mtu yoyote akifanya makosa ya jinai unaruhusiwa kukamata bila kuwa na hati.
Aliongeza kuwa, kumpinga Rais anapokosea sio kosa na kwamba tafsiri ya maneno aliyoyatoa ndio yamesababisha kukamatwa na kushitakiwa kwa kutumia lugha za kichochezi.
Lissu anadaiwa kuwa Juni 28, mwaka huu, akiwa katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alitoa kauli za uchochezi kuwa, “Mamlaka ya Serikali mbovu ni ya kidikteta uchwara inahitaji kupingwa na kila Mtanzania kwa nguvu zote, “huyu diktekta uchwara lazima apingwe kila sehemu”. Kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga nchi inaingia ndani ya giza nene.’’
Post a Comment