0
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sera na Mipango Ofisi ya Waziri Mkuu (bajeti) Bi. Grace Mosha akizungummza jambo wakati wa kikao cha tathimini ya utekelezaji wa mradi wa Kuimarisha Taarifa za Hali ya Hewa na Mifumo ya Tahadhari katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Meru Bw. Christopher Kazeri walipotembelea Wilaya ya Arumeru Arusha.
ARE2
Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha Bi.Maria Saidia akizungumza na Ti,mu ya ukaguzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotembelea kuona Utekelezaji wa Mradi wa wakati wa Kuimarisha Taarifa za Hali ya Hewa na Mifumo ya Tahadhari uliofunga mitambo ya kisasa ya taarifa za hali ya hewa Wilayani Arumeru mkoani Arusha.
ARE3
Muonekano wa Mitambo ya kisasa ya utoaji wa taarifa za hali ya hewa uliofungwa katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha ikiwa ni utekelezaji wa Mradi wa Kuimarisha Taarifa za Hali ya Hewa na Mifumo ya Tahadhari unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ufadhiri wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (United Nations Development Programme).
 (PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Wananchi wa Arumeru wameanza kunufaika na mradi wa Kuimarisha upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa na Mfumo wa Tahadhari unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kufungiwa mitambo ya kisasa ya kutoa taarifa za hali ya hewa na tahadhari.

Zaidi ya mitambo 40 imefungwa  nchi nzima ikiwa  Arumeru na Liwale ni moja ya wilaya za mfano ambazo mitambo hiyo imekuwa  ikisaidia Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kutoa taarifa za  utabili wa hali ya hewa  zenye uhakika na uharaka.

Mradi huo mpaka sasa umefanikiwa kufunga Mitambo katika maeneo ya Mbuguni, Hifadhi ya Taifa Arusha, Lyamungo, Manyara, Babati Longido, maeneo ya Bonde la Mto Pangani,Lushoto pamoja na Mombo
Wakizungumza na Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu waliofanya tathimini ya utekelezaji wa mradi huo,wakazi wa Arumeru wamesema tangu mitambo hiyo  ilipofungwa wamekuwa wanufaika wakubwa. 

“Sisi wakulima na wafugaji wa Mbuguni tumefaidika sana na uwepo wa mitambo ya kisasa ya utoaji wa taarifa za hali ya hewa katika maeneo yetu kwani kumesaidia wakulima kulima mazao yanayoendana na hali ya hewa na kuondokana na athari za mafuriko kwa kuzingatia taarifa za utabiri zinazotokana na mitambo iliyofungwa” alibaini Bi.Pepetua Mafia
Pamoja na hilo walikiri ongezeko la tahadhari kwa kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa imekuwa ikituma jumbe fupi za taarifa za utabiri wa hali ya hewa kwa maeneo yao katika simu za mkononi walizopewa na mradi huo.

“Tunafarijika na tunaona umuhimu wa taarifa za utabiri zinazotumwa katika simu hizi tulizopewa na mradi huu kwani imekuwa rahisi kujua vipindi mbalimbali vya hali ya hewa na kutusaidia kuweza kupanga shughuli za uzalishaji ikiwemo kilimo na ufugaji wenye tija ambapo kila baada ya siku kumi tunapokea jumbe kutoka Mamlaka ya hali ya hewa”alisisitiza mkazi wa Shambarai Bi.Elizabeth Laiza

Aidha pamoja na mafanikio hayo wakazi wa Arumeru waliomba Serikali kuongeza vituo na kujengewa uwezo zaidi ili kuepuka changamoto za uelewa mdogo wa taarifa za hali ya hewa.

“Tunaiomba Serikali itujengee uwezo zaidi juu ya umuhimu wa taarifa za hali ya hewa na tahadhari ili kutatua changamoto za kutojali taarifa hizo na kusaidia kuyakabili majanga ya mafuriko na ukame yanapotokea.” alisema Bw. Elibokea Lukio mkazi wa Maloloni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi masuala ya Bajeti Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Grace Mosha alipongeza jitihada zilizopo za waratibu wa  Ofisi yake kwa kushirikiana na wadau ikiwemo Wizara na Maji na Umwagiliaji Bodi ya Bonde la Mto Pangani, Wizara ya Kilimo na Mifugo na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini na kuwaomba kuendelea kutekeleza mradi huu ikiwezekana kuongeza mitambo hiyo kulingana na uhitaji.

“Niwapongeze wadau wote wa mradi kwani mradi umekuwa na matokeo chanya kwakuwa wananchi wamekiri na kuomba Serikali ifunge mitambo mingi zaidi ili kuifikia nchi nzima badala ya mitambo iliyopo sasa”.Alisisitiza Bi.Mosha

AWALI:Mradi wa Kuimarisha Taarifa za Hali ya Hewa na Mfumo wa Tahadhari ni mradi wa mfano na utekelezaji wake ni katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale mkoani Lindi na Arumeru mkoani Arusha ambapo umelenga kuwajengea uwezo wananchi katika kupata taarifa za tahadhari zitazosaidia kujiandaa, kukabili hali pindi unapotokea  Ukame na Mafuriko ikiwa ni maeneo yanayoathiriwa zaidi.Mradi huu ulianza kutekelezwa rasmi mwaka 2015 Ukiwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ufadhiri wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (United Nations Development Programme)

Post a Comment

 
Top