0
Katika maisha yetu ya kila siku hapa duniani kila mtu amewahi kukutana na hali ya kuumizwa na hata kuonewa juu eneo fulani, kiasi kwamba kujikuta akiona kila kitu hakiendi sawa na kufikia hali ya kushikilia jambo fulani alilofanyiwa na mwingine ndani ya moyo wake pasipo kuachilia. Hii si sawa kwa mtu yoyote mwenye malengo na maono makubwa kwa ajili ya maisha yake. Ni ngumu sana kuona uhalisi wa mafanikio unayoyataka kama utaendelea kushikilia mambo fulani uliyofanyiwa na mwingine pasipo kusamehe na kusahau.
Najua wapo watu kadhaa waliowahi kukutana na vitendo vya kubwaka yawezekana kabisa na ndugu au jamaa zao, wengine kukataliwa na wazazi wao, kufukuzwa kazi pasipo kutegemea, kutukanwa na kukejeliwa vibaya na watu wao wa karibu, kuumizwa kihisia katika mahusiano, kutengwa kijinsia au muonekano na mengineyo. Pamoja na hayo yote ni wazi kweli mambo hayo yanaumiza kisaikolojia na hasa pale unapofanyiwa na mtu wa karibu uliyemtegemea. Ni rahisi sana unapofanyiwa mambo kama hayo kujikuta ukishindwa kusamehe na kuachilia moyoni vitendo kama hivyo, na hili ndio limekuwa tatizo kubwa kwa watu wengi hadi sasa.
Mwalimu maarufu wa masuala ya kiroho na mafanikio kutoka nchini Marekani T.D Jakes aliwahi kusema, “Forgiveness is a gift you give yourself” (Msamaha ni zawadi unayoitoa kwako mwenyewe). Ni wazi kuwa unapotoa msamaha kwa jambo fulani ulilofanyiwa na mtu mwingine basi unakuwa unajitengenezea mazingira yako binafsi ya kujisaidia wewe kama wewe kuendelea mbele pasipo kukwama mahali. Haijalishi ni kosa la aina gani ulilofanyiwa na mwingine ila ni muhimu kuwa na utayari wa kusamehe kwa ajili ya faida yako binafsi.
Wakati mwingine tunaona makosa mengine tuliyofanyiwa ni makubwa sana hata kuona hatuwezi kusamehe, tumejikuta ni watu wenye uchungu kila tunapokumbuka mambo tuliyofanyiwa, na zaidi sana tumeibua hasira na chuki miongoni mwa watu waliotukosea hata kutafuta namna ya kulipa visasi juu ya adui zetu. Nataka nikuambie ukijifunza kusamehe na kuachilia kila unapokosewa, utakwepa mambo mengi sana mabaya yanayoweza kuambatana nawe. Hasira, uchungu, chuki, hofu, mashaka, maumivu makali, msongo wa mawazo, hisia zenye kuumiza, magonjwa ya moyo na hata kifo; yote hayo yanaweza kutokea kama hutoamua kusemehe na kusahau.
“As long as you don’t forgive, who and whatever it is will occupy rent-free space in your mind”
-Isabelle Holland
Kuna mstari mmoja katika kitabu cha biblia takatifu unaosema kuwa, “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka…” Naye Yesu Kristo ambaye ni mwalimu wa walimu alipata kuwafundisha wanafunzi wake kumi na wawili kuhusu habari ya msamaha kwa kuwaambia, “Kisha Petro akamwendea Yesu akamwambia, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Je, hata mara saba?” Yesu akamjibu, ‘‘Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.’’ Mahali pengine anaendelea kusema kuwa, “Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.” 
Nazani nimetumia Biblia zaidi kufundishia jambo hili kwa kuwa ndio kitabu pekee na kizuri sana kinachozungumzia habari za msamaha. Unahitaji kujenga tabia ya kusamehe waliokukosea haijalishi wamekutenda kosa la namna gani katika maisha yako. Unaposamehe na kuachilia unaufanya moyo wako na akili yako kuwa huru kwa ajili ya kuendelea mbele katika kutafuta mafanikio unayoyahitaji. Hakuna moyo wa kisasi uliowahi kufanikiwa. Jifunze kusamehe na kusahau kwa ajili ya maisha yako mwenyewe. Kama umeumizwa na wazazi wako kwa jambo lolote lile amua leo kuachilia ili utoe nafasi ya kuendeleza mahusiano mazuri na ya karibu kwao, hasa kwenye wakati unaoishi hapa duniani.
Mara nyingi moyo uliosamehe na kuachilia huwa ni dawa njema kwa ajili ya afya ya mwili na nafsi. Rafiki nakusihi samehe na kuachilia waliokukosea ili kuleta faida kwako, wawe ni wazazi wako, ndugu zako, rafiki zako, mfanyakazi mwenzako, au yoyote yule aliyekutenda vibaya amua kumsamehe na kumwachilia moyoni mwako kwa ajili ya faida yako binafsi ya kusogea mbele. Kila mtu anaweza kufanya kosa, hivyo fahamu kila binadamu ana mapungufu yake makubwa. Amini unaweza kumsamehe mtu aliyekukosea kama ukiamua kwa dhati kumsamehe na kusahau alichokutendea.
Leo kabla siku yako haijaisha kumbuka ni mtu gani ambaye umepoteza mahusiano nae ya karibu kabla ya hapo awali hajakukosea, amua kumtafuta kwa kumwandikia ujumbe mfupi wa maandishi (messages) au kuwasiliana nae moja kwa moja kwa simu na kumweleza juu ya uamuzi wako ulioamua kuuchukua kuanzia sasa wa kumtangazia msamaha. Mnaweza kupanga kukutana na mhusika mahali popote pazuri kama inawezekana kufanya hivyo.
Believe It’s Possible!

Post a Comment

 
Top