Na. Ahmad Mmow, Lindi.
Baraza
la halmashauri ya manispa ya Lindi, jana walikataa kupokea taarifa ya
tume iliyoundwa kuchunguza utekelezaji wa miradi iliyochini ya mfuko wa
maendeleo ya jamii wa mpango wa kuondoa umasikini (TASAF) katika
manispaa hiyo.
Walisema
miradi mingi inayotekelezwa kupitia mpango huo inatia mashaka. Hivyo
haikuwa sahihi kwa tume hiyo kuchunguza eneo moja wakati malalamiko yapo
katika miradi mingi na maeneo mengi.
Diwani
wa kata ya Mnazi mmoja, Said Mateva, alisema haikuwa sahihi tume hiyo
kuacha kuchunguza miradi inayolalamikiwa kila mara na iliyo wazi. Badala
yake imechunguza eneo moja tu kati ya mengi ambayo utekelezaji wake
unatia mashaka.
Alitolea
mfano kwenye kata yake kunafedha ziliendelea kulipwa kwa watu
waliofariki na wasionavigezo vya kunufaika na mpango huo. Hata hivyo wahusika hawajachukuliwa hatua hadi sasa. Ingawa amekuwa akilieleza jambo hilo ndani na nje ya baraza hilo.
"Mara
moja zilichukuliwa takribani shilingi lakimbili kwa ajili ya kununua
mafuta, wakati thamani halisi ya malipo yake ni shilingi 52,000 tu,
baada ya kupigwa kelele sana fedha hizo zilirejeshwa na kuingizwa kwenye
akaunti za vikundi. Kuna vikundi vinne vilipewa semina siku moja ndani
ya ukumbi mmoja, lakini wawezeshaji walijilipa posho ya siku nne, yote
hayakuchunguzwa".
Mateva
aliutaja mradi mwingine unaotia mashaka ni kilimo cha umwagiliaji kwa
njia ya matone. Akibainisha kwamba hata njia zilizotumika kumpata
mzabuni wa ujenzi wa tangi zinatia mashaka. Diwani wa kata ya Mitandi,
Hafidh Kitutu alisema mpango wa serikali wa kuziondolea umasikini kaya
zisizo na uwezo katika halmashauri hiyo hautafanikiwa iwapo hali
itaendelea kuachwa bila kudhibitiwa.
Hivyo
kunahaja ya kuundwa tume nyingine itakayochunguza miradi yote
inayotiliwa mashaka na kulalamikiwa na wananchi. Maelezo ya madiwani hao
yaliungwa mkono na diwani wa kata ya Mtanda, Abeid Bakari aliyewashauri
madiwani wenzake wasipokee taarifa hiyo. Kwani licha ya kuwa na ya
eneo moja, lakini pia hawakupewa mapema kabla ya kikao hicho
iliwaisome.
Ambapo
diwani wa kata ya Ndolo, Issa Luono aliwaeleza madiwani wenzake
wasiogope gharama wakubali kuunda tume nyingine na waachane na taarifa
iliyokuwa mbele yao.
"Ukitaka
kumpa talaka mke usiogope hasara wala gharama ulizotumia kwake,
ukijuliza hayo huwezi kumuacha, utazidi kuumia, utaendelea kupata karaha
na hasara. Tuunde tume nyingine wala hatumtafuti mtu bali tunatekeleza
wajibu wetu kwa wananchi," alisema Luono.
Kwa
upande wake mkurugenzi wa manispaa hiyo, Jomaary Satura licha ya kusema
hakuwa na kipingamizi kuhusu kuundwa tume nyingine. Hata hivyo
aliwatahadharisha na kuwaasa madiwani hao kwamba tume hizo zinatumia
fedha za wananchi. Hivyo wasiunde kwa ajili ya kujinufaisha.
Alisema
ni jambo la kushangaza kuona madiwani hao wanakataa kupokea taarifa
wakati mwenyekiti wa kamati ya fedha, ambae pia ni makamo meya wa
halmashauri hiyo alizungukia miradi yote wala hakukosoa taarifa hiyo.
"Nakamati
ya fedha ni kubwa kuliko hizo tume zinazoundwa". Satura aliendelea
kuwaasa madiwani hao kuangalia maudhui na athari za kuunda tume mara kwa
mara na miradi wanayokwenda kukagua.
Hata
hivyo maelezo ya mkurugenzi huyo na ya meya wa halmashauri hiyo,
Mohamed Lihumbo aliyeshauri taarifa hiyo ipelekwe na kujadiliwa kwenye
kamati ya fedha hayakubadili msimamo wa madiwani hao. Hivyo taarifa hiyo
haikupokelewa na ilikubalika iundwe tume nyingine.
Post a Comment