Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameitaka Mamlaka
ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kusitisha bei mpya ya umeme
iliyotangazwa juzi na Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Felix Ngamlamgosi.
Taarifa ya kusitisha kwa bei hiyo ilitolewa jana na Profesa Muhongo kupitia barua yake kwa Ewura.
Muhongo amesema kuwa amesitisha bei hiyo mpya kwa sababu nne, ikiwamo
kutoshirikishwa katika mchakato huo akiwa ni waziri mwenye dhamana.
“Ewura walipokwenda mikoani Watanzania wote walipinga bei kupanda, wao
wametumia kigezo kipi cha kupandisha? Pili taratibu zilizopo ni kwamba
Tanesco wanapeleka maombi Ewura, kisha Ewura wanafanya zoezi hilo la
kuuliza wahusika watumiaji wa umeme, baada ya hapo wanatengeneza ripoti
wanaileta wizarani, na ningaliipata hiyo ripoti.
“Hivi tunavyoongea sijaipata mkononi, nikiipata nitaiita Ewura na
Tanesco tunajadili na baada ya hapo ndipo wanaenda kutangaza. Wao
wametangaza hata mimi taarifa nazipata kama wewe,” alisema Profesa
Muhongo.
Katika sababu ya tatu ya kusitisha bei hiyo, Profesa Muhongo alisema
hakuna ukweli kuwa kupandisha bei ya umeme kutasababisha Tanesco imalize
matatizo yake kifedha.
“Tanesco kila mwaka inapandisha bei, mbona hawajajikwamua? Mbona madeni
yanazidi kuongezeka? Nyingine ni kwamba tunakopa fedha kutoka nje ya
nchi na watakaolipa hilo deni ni Watanzania wote, sasa hatuwezi kukopa
kulipa madeni ya Tanesco halafu shukrani tutakayoipata ni kupandishiwa
bei ya umeme tena.
“Nyingine nenda ufuatilie Tanesco wana matumizi mabaya ya fedha,
nimesitisha zoezi lao, sijui kama hizo fedha wamerudisha, unajua
wanapeana wale walioko juu bonasi kati ya Sh milioni 40 na milioni 60
kwa mwaka,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema Ewura wanapaswa kupeleka ripoti ijadiliwe, kwani haiwezi kuwa
Serikali ndani ya Serikali na haiwezi kupandisha bei bila waziri mwenye
dhamana kujua kwa kuwa inapata bajeti kutoka bungeni.
Post a Comment