OFISA
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Kapteni Keenan
Mhaiki, amefariki dunia jana saa 5:25 asubuhi katika Hospitali ya Agha
Khan Jijini Dar es Salaam.
Alilazwa katika hospitali hiyo Alhamisi iliyopita, kabla ya sikukuu ya Krismasi, kwa ugonjwa wa saratani ya ini.
Kaka
mkubwa wa marehemu, ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya
Sheria, Oliver Mhaiki alisema hayo jana alipokuwa akizungumza nasi.
Mhaiki
alisema Kapteni Keenan ambaye ameendesha marais wa awamu zote tano,
alianza kuumwa Julai mwaka huu kwa kusumbuliwa na pingili ya ‘lumber’,
hali iliyoelezwa na madaktari ni kwa sababu ya kukaa muda mrefu.
Alisema
marehemu alikuwa akisumbuliwa na maumivu na Oktoba mwaka jana
alipokwenda India kwa ajili ya uchunguzi zaidi, ndipo baadaye alirudi
kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.
“Kilichomuua
sio hicho, inaonekana alikuwa na saratani ya ini muda mrefu,
hakuigundua, hivyo wiki mbili zilizopita alibadilika rangi kuwa njano,
alipoenda hospitali wakagundua ni saratani,” alisema kaka huyo wa
marehemu.
Alisema
marehemu ameacha mke na watoto wawili na kwamba anatarajiwa kuzikwa
Songea. Alisema hivi sasa wanasubiri wadogo wa marehemu waliopo nje ya
nchi.
Alisema katika familia yao, wamezaliwa watoto nane.